1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya jana baina ya Marekani na Iran huko Baghdad hayajafua dafu

Marekani na Iran hazina uhusiano rasmi wa kibalozi, lakini ilivokuwa sasa mambo hayamuendei uzuri Rais George W. Bush wa Marekani huko Iraq, nchi hizo mbili sasa zinazungumza pamoja, japokuwa katika ngazi za mabalozi tu na japokuwa kwa nadra.

Balozi wa Marekani katika Iraq, Ryan Crocker

Balozi wa Marekani katika Iraq, Ryan Crocker

Mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, mabalozi wa nchi zote mbili mjini Baghdad, Ryan Crocker na Hassan Kasemi Komi, walikutana kwa mara ya kwanza kuzungumzia juu ya usalama wa Iraq. Lakini hawajafakia maendeleo makubwa katika mazungumzo hayo. Jana walirejea tena kwa mara ya pili, na pia , kwa mujibu wa balozi wa Kimarekani, hamna mengi yalioambuliwa.

Ni tu matokeo yanayohesabiwa na sio nia. Hivyo ndivyo alivosema balozi wa Marekani mjini Baghdad, Ryan Crocker, baada ya kuwa na mazungumzo ya pili na mwenzake wa Iran katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Kile kilichozungumziwa kwa masaa, mtu angeweza kukizungumza kwa dakika chache. Na tangu yale mazungumzo ya mwanzo ya Mei 28, mambo huko Iraq yamekuwa mabaya zaidi kuliko kuwa mazuri.

Sura ilioko sasa Iraq haijatoa utabiri mzuri kwa mazungumzo ya jana, lakini hadithi haijamalizika bado. Baada ya karibu miaka 30 ya ukimya baina ya Washington na Tehran, mtu asistaajabu kwamba mwanzo huu mpya ni mgumu. Na hasa ilivokuwa malengo ya mazungumzo yenyewe sio kuurejesha tena uhusiano wa kibalozi baina ya nchi hizo mbili, uliovunjika muda mfupi baada ya kufanyika Mapinduzi ya Kiislamu, au kutafuta suluhisho la mzozo wa kinyukliya baina ya nchi hizo mbili. Suala pekee la mazungumzo ya jana, japokuwa ni suala moto, ni hali ya mambo ilivyo huko Iraq.

Hili ni suala ambalo, licha ya pande zote mbili kujitia huku na kule, tayari pande hizo zamani zimeshatambua kwamba, kimsingi, zina maslahi ya aina moja na inafaa zishirikiane. Yaani ikiwa zinataka kuvikiuka vivuli vyao wenyewe. Iran inaweza tu kuridhika pindi itaiona Iraq inakuwa tulivu kwa upesi, na kwamba nchi hiyo ya mito ya Euphrates na Tigris inakuwa jirani wa amani, hivyo kuwa sio tena kitisho zaidi kwa Iran. Lengo la Marekani pia sio tafauti na hilo, japokuwa kunawekwa alama ya kuuliza kama njia inayofuata inaelekea katika lengo hilo.

Yanayofanywa na Marekani yameisaidia Iran huko Iraq, kama vile ilivofaidika hapo kabla huko Afghanistan. Katika nchi zote mbili tawala za siasa kali zimepinduliwa, nchi ambazo zinapakana na Iran. Iran iliokuwa hasimu wa mahasimu, haijabadilika kuwa mshirika wa Marekani, kwa hakika haijabadilika kuwa nchi rafiki. Huu ukimya uliokubaliwa kuweko baina ya Washington na Tehran ndio jambo lililowezekana kwa kiwango cha juu kabisa. Na hali hiyo imemalizika zamani, tangu pale Marekani ilipozidisha mbinyo kwa Iran kutokana na mabishano yao juu ya mradi wa Tehran kutaka kuwa na nishati ya kinyukliya. Kwa Iran, Marekani sio tena shetani mkubwa wa kutokea Bahari ya Atlantik, lakini ni adui aliye mlangoni na ambaye mara nyingi hutishia kwamba anaweza kwa urahisi kuishambulia Iran kutokea Iraq na pia Afghanistan ili kuupinduwa utawala wa mashehe wanaouchukia au angalau kuviangamiza vinu vya kinyukliya vya Iran.

Kile ambacho lazima kiwatie wasiwasi Wa-Iran kimegeuka, wakati huo huo, kuwa afuweni kwa wananchi wa Iran. Marekani hivi sasa imo kwenye shida katika nchi jirani, yaani huko Iraq na Afghanistan, hata kufanya isiweze kuvipanua vita hadi Iran. Sababu ni hali halisi ilivyo katika eneo hilo la mapigano na kutokana na sababu za siasa za ndani za huko Marekani. Vita vinavoendelea Iraq vimewezesha kile kitisho ilichokuwa nacho Iran dhidi ya Marekani, yaani maroketi yake ya masafa marefu kuonekana kuwa ni jambo la kipuuzi. Iran, kupitia washirika wake huko Iran inaweza kuendesha upinzani na kuyafanya maisha kuwa magumu kwa Wamarekani huko Iraq, hata bila ya kutumia maroketi hayo.

Marekani inasema Iran tangu hapo inatumia mkakati huo, lakini Iran inabisha. Hata hivyo, pande hizo mbili zinataka kuunda mkakati wa pamoja wa usalama. Kwa hivyo mkutano wa jana wa Baghdad haujawa kazi ya bure.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com