1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayochipukia kiuchumi yataka kuzingatiwa

Tuma Provian Dandi22 Oktoba 2007

Wakati nchi zilizoendelea kiviwanda zikitafakari hali ya uchumi unaotikisika, mataifa yanayochipukia kiuchumi yametaka kuthaminiwa na mashirika ya kimataifa badala ya kukumbatia nchi tajiri zilizo katika kundi la G7

https://p.dw.com/p/C77a
Baadhi ya Mawaziri na Maofisa kutoka Wizara za Fedha za nchi wanachama wa G7
Baadhi ya Mawaziri na Maofisa kutoka Wizara za Fedha za nchi wanachama wa G7Picha: AP

Mataifa mbalimbali yaliyoanza kupata mafanikio kiuchumi ambayo hayakuathiriwa na mikopo kutoka mashirika ya kimataifa, yameyataka mataifa tajiri yenye mafanikio viwanda hasa yale yaliyoathiriwa na mikopo, kutambua juhudi zao katika masuala ya uchumi.

Tamko la mataifa hayo yanayochipukia limekuja wakati ambapo nchi tajiri kutoka kundi la G7 zikitafakari madhara yalitokea hivi karibuni baada ya uchumi wa nchi hizo kutikisika hasa zile zilizochukua mikopo ya majumba.

Nchini Marekani madhara ya kutikisika kwa uchumi yamejitokeza baada ya makampuni yaliyochukua mikopo ya majumba kutoka kwa masharika ya fedha ya kimataifa kushindwa kufanya kile kilichokusudiwa, hali iliyosababisha hatari katika uchumi wa nchi hiyo.

Waziri wa Fedha wa Brasil Guido Mantega amenukuriwa akisema kwamba nchi zilizokuwa zikiheshimika kutokana na uchumi wake hivi sasa zinahaha huku zikitafakari ni wapi zilipokosea baada ya kuchukua mikopo mikubwa kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa.

Waziri huyo amesisitiza kwamba kwa nchi kama Brasil ambazo zinaibukia kiuchumi bila kupitia mikopo kama ile iliyochukuliwa na Marekani na nchi kadhaa za Ulaya, zinapaswa kupewa kipaumbele wakati huu ili kuzidisha juhudi zake katika kukuza uchumi na kustawisha maisha ya watu wake.

Awali Waziri huyo wa Fedha wa Brazil anayetarajiwa kuchukua Uenyekiti wa nchi 20 zinazochipukia katika uchumi mwezi ujao, alitaraji kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wa Marekani Bwana Henry Paulson ambapo pamoja na mambo mengine, angetia msukumo wa kutambuliwa kwa mataifa yanayochipukia bila kuathiriwa na mikopo kutoka kwanye taasisi za kimataifa.

Mazungumzo hayo pia yanalenga kufikia ushirikiano wa karibu kati ya nchi tajiri na zile zinazochipukia pamoja na kuyataka mashirika makubwa ya fedha kutoa udhamini kwa mataifa yanayoendelea.

Ama kutokana na hitilafu ya kiuchumi iliyozikumba nchi wanachama wa kundi namba saba maarufu kwa jina la G7, tayari mawaziri kutoka mataifa hayo wamekuwa takifanya tathmini ya mtikisiko wa uchumi uliowakumba siku za hivi karibuni.

Nchi hizo ni Marekani, Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia pamoja na Japani.

Wakati zikijiuliza juu ya hitilafu hiyo la uchumi, nchi hizo kwa sasa zinatafakali juu ya mataifa yanaochipukia ikiwemo Brasili, India, China na Afrika Kusini.

Hata hivyo kundi hilo la G7 limesema pamoja na hali iliyotokea ikiwemo kupanda kwa gharama za mafuta, uhaba wa masoko na tatizo la mikopo ya majumba, nchi hizo zimesema zitahakikisha zinakuwa kileleni katika medani ya uchumi na kwamba zitaendelea kuziba mianya iliyosababisha mtikisiko wa uchumi katika kipindi kifupi kilichopita.

Kitu kikubwa kinachozisaidia nchi wanachama wa kundi namba 7 yaani G7 kuwa na maendeleo makubwa, ni ushawishi mkubwa zilionao kwa mashirika ya fedha ya kimataifa hasa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, tofauti na mataifa yanayochipukia ambayo hufanya kazi ya ziada ili kupata mikopo mikubwa kama ile ya majumba inayotolewa kwa Marekani na nchi nyingine za barani Ulaya.