1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yailaumu Iran kujihusisha na machafuko Iraq

Charles Mwebeya12 Februari 2007

Kwa mara ya kwanza maofisa wa kijeshi wa Marekani wamesema wana ushahidi kuwa Iran imekuwa ikitoa silaha na mabomu kwa vikundi vya wamamgambo wa kishia wanaoleta machafuko nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/CHKO
Nejad akihutubia taifa katika maadhimisho ya 28 ya Mapinduzi ya Iran.
Nejad akihutubia taifa katika maadhimisho ya 28 ya Mapinduzi ya Iran.Picha: AP

Katika taarifa iliyotolewa jana mjini Baghdad maofisa hao walionyesha vifaa kadhaa vya kijeshi kama vile mabomu yenye namba za Iran.

Maofisa hao wamesema kuwa mnamo mwaka 2005 nchini Iraq , waliikamata meli iliyokuwa na shehena ya silaha kutoka Iran.

Pia wameongeza kuwa vikosi vya usalama vya Iran vimekuwa vikipeleka silaha nchini Iraq, ambazo lengo likiwa ni kuwaangamiza wanajeshi wa Marekani pamoja na maafisa wa ngazi za juu nchini Iraq.

Taarifa hiyo, imeongeza kuwa shughuli zote za kusafirisha silaha kutoka Iran kwenda Iraq zimekuwa zikiratibiwa na viongozi wa juu wa serikali ya Iran.

Taarifa hiyo ya Jeshi la Marekani inasema kuwa toka mwezi June mwaka 2004 mpaka hivi sasa , jumla ya wanajeshi wake 170, wameuawa na milipuko ya mabomu yaliyotengenezwa ama kusafirishwa kutoka Iran.

Hata hivyo katika mkutano huo waandishi wa habari hawakuruhusiwa kupiga picha wala kurekodi tukio lolote.

Kikosi cha Al – Quids, mojawapo ya vikosi vya ulinzi katika jeshi la mapinduzi nchi Iran kimehusishwa na shutuma hizo . Kiongozi wa kikosi hicho alikamatwa na majeshi ya Marekani Mwezi January mwaka huu katika machafuko yaliyotokea katika mji wa Irbil huko Iraq.

Machafuko ya mara kwa mara nchi Iraq , yamekuwa ni kikwazo katika kuleta hali ya usalama na amani nchini humo, pamoja na kuwapo kwa vikosi vya kulinda amani kutoka Marekani.

Wakati huo huo viongozi wa chama cha Demokratik huko Marekani wamemtaka Rais George Bush kuwa muangalifu katika shutuma hizo dhidi ya Iran.

Mmoja wa maseneta wa chama hicho Chris Dodd amesema ripoti iliyotolewa na maafisa wa kijeshi wa Marekani huko Iraq, ina walakini na isije ikatumika kama mbinu ya kuivamia Iran Kijeshi.

Wakati hayo yakijiri, mawaziri 27 wa mambo ya nchi za nje wa jumuiya ya ulaya wanakutana leo mjini Brussels, huku mojawapo ya ajenda ikiwa ni tamko la Rais wa Iran Mohamoud Ahmednejad kutangaza hapo jana nchi yake kuendelea na na mpango wa kinyuklia .

Nejad akilihutubia taifa hapo jana katika maadhimisho ya 28 ya siku ya mapinduzi ya Iran, amesema Iran itaendelea na mpango wake wa kinyuklia bila kuhusisha kazi za kiatomi.

Hata hivyo Rais huyo wa Iran yuko katika shinikizo kubwa nchini mwake kutokana na kauli hiyo , ambayo inaungwa mkono na baadhi ya wananchi , huku wengine wakiipinga.

Na taarifa za hivi punde kutoka mjini Baghdad zinasema kuwa watu wawili wameuawa na mlipuko wa bomu, uliotokea kwenye soko moja katikati ya mji huo.

Mlipuko huo uliotokea katika soko la Shorja , soko ambalo limekumbwa na matukio ya milipuko ya mabomu mara kwa mara, umesababisha moshi mkubwa katikati ya anga, mjini Baghdad mchana huu.