1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yadhamiria kujenga kituo cha Kijeshi Afrika

Isabella Mwagodi7 Februari 2007

Rais wa Marekani George W. Bush ameuidhinisha mpango wa kujenga kituo cha kijeshi cha Afrika. Hatua hii inadhihirisha wasiwasi wa Marekani dhidi ya ongezeko la visa vya ugaidi katika maeneo mbalimbali ya Afrika pamoja na kuvutiwa na raslimali ya bara hilo.

https://p.dw.com/p/CHKb
Rais George Bush
Rais George BushPicha: AP

Maamuzi ya rais Bush yametokana na mjadala kuhusu matukio ya majeshi ya Kiislamu kujaribu kumiliki maeneo mbalimbali ya bara la Afrika. Katika taarifa yake rais huyo alisema hatua hii pia itawezesha Marekani kudhibiti mahusiano ya kiuslama na pia kuimarisha nafasi za wawekezaji.

Nchini Ujerumani,msemaji wa majeshi ya Marekani, Holly Silkman, aliliambia gazeti la Stuttgarter Zeitung ,kuwa shughuli za kituo hicho Africom zitaendeshwa katika kambi ya kijeshi la Kelly, mjini Stuttgart, na baadaye kuhamishiwa katika kituo cha Afrika katika siku zijazo,mipango itakapokamilika.

Tayari maafisa wa Marekani wameanza kuhamisha vyombo vya kutekeleza mradi huo wa Africom mjini Stuttgart.

Kulingana na mazungumzo baina ya rais Bush na waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates, kituo hicho cha kijeshi cha Africom, kinatarjiwa kuhamishwa katika bara la Afrika,mwezi Septemba mwaka 2008.

Marekani imesema inafanya majadiliano na viongozi wa Afrika kuchagua eneo mwafaka,ambapo kituo hicho kitajengwa.

Kwa kawaida,jeshi la Marekani hutuma vikosi vyake kuendesha shughuli za usalama katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Kwa mfano, Kituo cha Central Command husimamia eneo la Mashariki ya kati,na Pembe ya Afrika. Serikali ya Marekani imesema,Kituo hiki cha Africom kitawawezesha kushuguhulikia kwa kina Africa kuliko ilivyo hivi sasa ambapo Afrika inasimamiwa na kituo cha kijeshi cha Kati na Ulaya,mpango ambao ulianzishwa wakati wa vita baridi.

Hatua hii imezusha mjadala kuhusu nia ya Marekani barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni. Hasa katika serikali ambazo hazina uwezo mkubwa wa kujidhibiti na visa vya ugaidi. Mtandao wa Al Qaeda uliendesha shambulio la ugaidi katika ubalozi wa Marekani jijini Nairobi-Kenya,na Dar e Salaam Tanzania, katika mwaka wa 1998,na kuwauwa zaidi ya watu 250. Hivi majuzi Marekani iliyashambulia maeneo yaliodaiwa kuwa ni maficho ya makundi ya Al Qaeda katika nchi ya Somalia. Marekani pia ilianzisha vituo vya kutoa mafunzo ya kupambana na magaidi Magharibi na Afrika ya kati mwaka 2002,ili kuwafundisha wanajeshi jinsi ya kuwawinda magaidi.

Lakini pia Marekani ina tamaa ya rasilmali ya nishati ya bara la Afrika,ikionekana kama njia ya kupunguza kutegemea nishati kutoka eneo la Mashariki ya kati. Marekani,ina matumaini kwamba Ukanda wa Guinea katika Afrika Magharibi, utawapa angalau robo ya mahitaji yao ya nishati. Si ajabu wamekazana na juhudi za kudhibiti usalama barani Afrika ili kufanikisha mipango yao ya kupata nishati kwa urahisi.