1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Iran zote zalaumiwa kwa kinachotokea Iraq

Saumu Mwasimba29 Machi 2007

Waarabu wengi wanaamini kwamba dhima ya Iran na Marekani nchini Iraq ni mbaya.

https://p.dw.com/p/CHHB
Picha: AP

Waarabu wanaamini dhima ya Marekani Iraq ni mbaya na kwahivyo wanaitaka nchi hiyo kuondoa majeshi yake haraka iwezekanavyo.Iran pia inanyooshewa kidole cha lawama juu ya hali tete kwenye eneo hilo.

Hayo yamebainika katika uchunguzi wa maoni uliofanywa kwenye mataifa matano ya kiarabu

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na na taasisi ya masuala ya nchi za kiarabu na Marekani AAI pamoja na taasisi ya kimataifa ya Zogby , wananchi kutoka mataifa ya Misri,Saudi Arabia,Jordan ,Emarati na Lebanon wanailaumu Marekani pamoja na Iran kwa majukumu yao ambayo yamechangia hali mbaya nchini Iraq.

Maoni ya wananchi wengi katika nchi hizo yanaashiria kuinyooshea kidole cha lawama Iran katika kile kinachotokea kwenye eneo hilo tangu vita vya Israel na Hezbollah.

Mkuu wa taasisi ya AAI James Zogby anasema ni wazi rais wa Iran Mahmoud Ahmednejad ameleta hali ya wasiwasi katika eneo hilo na kuimeza kabisa nia njema iliyojengwa na Iran hasa baada ya rais huyo kuliunga mkono kundi la Hezbollah na kuipinga Marekani na Israel,bila ya kuweka kando majigambo ya Iran katika mpango wake wa Kinuklia.

Wasiwasi mkubwa wa wananchi juu ya Iran umejitokeza zaidi nchini Saudi Arabia ambako wengi wa wale waliohojiwa walisema dhima ya Iran nchini Iraq ni mbaya zaidi kuliko ile ya Marekani nchini humo.

Asilimia 78 ya wasaudi wameiponda Iran wakati ni asilimia 68 nchini humo ilidiriki kusema Marekani ndiyo ya kulaumiwa kwa hali nchini Iraq.

Lakini wasiwasi huo juu ya Iran ulizungumziwa tofauti katika nchi za Misri na Jordan.

Nchini Misri kwa mfano asilimia 83 ya watu walioulizwa waliitaja Marekani kuwa yenye dhimka mbaya nchini Iraq ikilinganishwa na ailimia 66 ya watu walioilaumu Iran kwa jukumu lake Iraq.

Jordan asilimia 96 waliilaumu moja kwa moja Marekani juu ya hali ya Iraq huku asilimia 73 ikisema Iran pia inabeba dhamana.

Watu 3,400 walihojiwa katika utafiti huo kutoka nchi hizo tano za kiarabu kati ya mwezi Februari na mapema mwezi Marchi.

Utafiti huo pia umebainisha kuwa kuwa wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa Iraq kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Idadi kubwa ya watu waliohojiwa katika mataifa hayo walisema hofu yao kubwa ni kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenywe Iraq na kusambaa hadi kwenye maeneo ya mipaka ya nji jirani au hata nchini hiyo kugawika pande tatu.

Utafiti huu mpya unafuatia utafiti mwingine uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Zogby nchini Misri,Jordan,Lebanon,Saudi Arabia na Morcco mnamo mwishoni mwa mwezi wa Novemba na Desemba.

Taasisi hiyo ya Zogby inaendeshwa na nguguye James Zogby.

Tafiti hizo mbili zimebainisha kuwa sio tu Kujiingiza kwa Marekani kwenye ulimwengu wa kiarabu ndiko kulikoleta matatizo kwenye eneo hilo bali hata Iran inabeba msalaba huo wa lawama kwa kukiunga mkono Kikundi cha Hezbollah huko Lebanon na ukaidi wake dhidi ya Marekani.

Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa na taasisi hizo umeonyesha kwamba nchi nne kati ya hizo tano raia wanasema juhudi za Marekani za kuzuia mpango wa Kinuklia wa Iran zimechangia mtazamo wao mbaya kuelekea Marekani.

Uchunguzi huo umeungwa mkono na Prof Shibley Telhami wa chuo kikuu cha Maryland ambaye ni mtaalamu wa masuala ya umma ya nchi za kirabu.

Watu sita kati watu kumi waliohijiwa kwenye utafiti huo walisema wanaamini Iran ina haki zote za kutafuta technologia ya Kinuklia hata ikiwa taifa hilo la kiislamu linania ya kutengeneza sialaha za kinuklia.

Ni wachache tu waliosema kwamba mpango wa kinuklia wa Iran unastahili kuzuiwa.

Lakini cha ajabu zaidi katika nchi hizo watu waliohojiwa wakiulizwa kutaja vitu viwili ambavyo wanahisi ni tisho kubwa kwa usalama wan chi zao takriban asilimia 80 walizitaja Israel na Marekani.