Marekani itaendelea na mradi wa kinga barani Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.06.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani itaendelea na mradi wa kinga barani Ulaya

Marekani haitaki kuachilia mbali mpango wake wa kujenga vituo vya kujikinga dhidi ya makombora katika Ulaya ya Kati,licha ya Urusi kupendekeza kuwa pamoja zitumie rada za nchini Azerbaijan.

Makao makuu ya NATO mjini Brussels

Makao makuu ya NATO mjini Brussels

Waziri wa ulinzi wa Marekani,Robert Gates alieleza msimamo wa nchi yake alipokutana mjini Brussels na mawaziri wenzake wa Shirika la Kujihami la NATO na pia waziri wa ulinzi wa Urusi,Anatoly Serdyukov.

Mawaziri wa ulinzi wa NATO hawaoni sababu ya kubadilisha mipango ya Marekani ya kutaka kujenga vituo vya kujikinga dhidi ya makombora.Hata baada ya Urusi kupendekeza kuwa Marekani inaweza kutumia kituo cha rada nchini Azerbaijan pamoja na Urusi,waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates anataka kuendelea na majadiliano yake pamoja na wanachama wenzake wa NATO yaani Poland na Jamhuri ya Czech.Kuambatana na mipango ya Marekani,nchini Poland kutajengwa kituo cha kurusha roketi za kuzuia makombora.Na nchini Jamhuri ya Czech ndio kutawekwa mtambo wa rada wa kituo hicho.

Katibu Mkuu wa NATO,Jaap de Hoop Scheffer amesema,haamini kuwa pendekezo lililotolewa na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Heiligendamm kuhusu kituo cha rada nchini Azerbaijan,ni mradi mbadala au mpango huo utachukua nafasi ya majadiliano ya pande mbili yaani kati ya Marekani na Poland na vile vile pamoja na Jamhuri ya Czech.

Scheffer akaongezea kuwa pendekezo la Urusi kwamba Marekani ishirikiane na Urusi kusimamia sehemu ya mfumo huo wa kujikinga,hudhihirisha kuwa sasa hata Urusi inatia maanani kitisho cha roketi kutoka Iran.

Wakati huo huo shirika la NATO hadi mwaka 2008 linataka kuchunguza ikiwa mipango yake ya kujikinga dhidi ya makombora itaweza kufungamanishwa na mradi wa Marekani.Mpaka sasa, ni hasa sehemu za Ulaya ya kusini-mashariki zisizokuwa na mfumo wo wote ule wa kinga.

Kwa maoni ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani,Franz Josef Jung suala hilo lakini lisisababishe mtengano wo wote barani Ulaya.Akiendelea alisema, ni lazima kwa wote barani Ulaya kutaka kujenga mfumo wa kinga kwa ajili ya umma kwa jumla

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com