1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti na Abdu Mtullya

2 Novemba 2006

Jee Ujerumani itumie vipi mapato yanayotokana na kodi na kwa muda gani majeshi ya Ujerumani yataendelea kuwapo nchi za nje? Hayo ndiyo masuala yanayozingatiwa leo na wahariri wa magazeti katika maoni yao.

https://p.dw.com/p/CHUY

Gazeti la LAUSITZER RUNDSCHAU kutoka mji wa Cottbus mashariki mwa Ujerumani. Linazungumzia juu ya wazo la waziri wa ulinzi wa Ujerumani bwana Franz Joseph Jung kuhusu kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa nchi hii waliopo Bosnia. Mhaririwa gazeti hilo anasisitiza kuwa waziri huyo ana haki kabisa ya kutoa wazo hilo.

Anatilia maanani kuwa jukumu kuu la wanajeshi ni kusaidia katika sehemu za mizozo na ikibidi kuingilia kati ili kuzima mizozo hiyo. Pia anatilia maanani kwamba wanapopelekwa katika kutekeleza majukumu hayo, askari hao pia hupewa muda maalamu. Na hivyo basi hawawezi kuwa mbadala wa polisi wa nchi inayosaidiwa . Lazima waondoke baada ya muda fulani.

Lakini mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE kutoka mji wa Potsdam pia mashariki mwa Ujerumani ana mashaka juu ya tathmini ya waziri wa Ulinzi bwana Jung, kwamba wakati sasa umefika wa kuwarudisha nyumbani askari wa Ujerumani waliopo Bosnia.

Mhariri huyo anahoji kuwa waislamu,waserbia na wakroatia wanawalikishwa na viongozi wenye misimamo mikali, na polisi inayopaswa kuchukua jukumu la majeshi ya kimataifa bado haijaonekana, Hivyo basi gazeti linasema hali bado haijakuwa ya kutengemaa.

Mhariri wa gazeti la VOLKSSTIMME anasema kuwa kuwarejesha nyumbani askari hao kwa sababu tu mambo fulani yameenda mrama hakutasaidia bali kutaathiri sifa ya Ujerumani katika utekelezaji wa majukumu ya kimataifa.

Katika tahariri zao wahariri wa magazti leo pia wanatoa maoni yao juu ya mkutano wa viongozi wa serikali utakaofanyika kesho kujadili jinsi ya kutumia fedha zaidi zinazoingia kutokana na makusanyo ya kodi.

Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linasema , ghafla tu mifuko imejaa fedha.!Lakini hakuna furaha juu ya fedha hizo.

Sababu mojawapo anaeleza mhariri wa gazeti hilo ni kwamba wahusika yaani wananchi hawaulizwi juu ya hayo,;sababu ya pili anasema mhariri serikali ina mipango chungutele lakini haina mkakati wowote.

Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE linaikumbusha serikali kuwa manmo mwaka huu vilevile imeendelea kukopa na inazidi kulimbikiza mzigo wa riba kwa vizazi vijavyo. Hivyo basi anashuuri kuwa ,mwenye deni la Euro mia ajaribu kuiweka katika akiba Euro kumi anayookota. Na litakuwa jambo la busara ikiwa fedha hizo zinazotokana na makusanyo zitaekezwa katika vitenga uchumi.