1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maalfu ya wakimbizi wametoweka

Admin.WagnerD30 Agosti 2016

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya kutoweka kwa maalfu ya watoto wa wakimbizi nchini Ujerumani. Na pia wanaeleza kwa nini Uturuki haitaki kuona nchi ya Wakurdi ikiundwa.

https://p.dw.com/p/1JsJu
Watoto wa wakimbizi nchini Ujerumani
Watoto wa wakimbizi nchini UjerumaniPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Polisi ya Ujerumani imesema kwamba idadi ya watoto wa wakimbizi waliotoweka nchini imeongezeka mara mbili. Na wengi miongoni mwao ni wale wenye umri wa kati ya miaka 14 na 17. Idara kuu ya kupambana na uhalifu imesema sababu ya watoto hao kutoweka ni hitilafu zinazotekea wakati wa kusajiliwa.

Mhariri wa gazeti la "Märkische Oderzeitung" anakubaliana na maelezo hayo na anasema si kila mkimbizi anakwenda kule anakopangiwa kwenda.Wengi wanaondoka mashambani na kwenda miji mikubwa. Na wengine huenda katika nchi jirani.

Lakini pamoja na maelezo ya idara za serikali, mhariri wa gazeti la "Märkische Oderzeitung" anashauri kuweka utaratibu wa kuwapeleka wakimbizi vijana na watoto kule wanakotaka kwenda kuungana na jamaa zao, mara tu baada ya kuwasili nchini.

Mhariri huyo anasema utaratibu huo utawezesha kupatikana kwa maafisa wa kutosha kwa ajili ya kuwatafuta wale watoto ambao kweli wametoweka.

Majeshi ya Uturuki yaendelea kuwashambulia Wakurdi

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linasema lengo la operesheni ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mwa Syria, ni kuzuia kuundwa kwa nchi ya Wakurdi. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kuundwa kwa nchi hiyo kutakuwa kama ndoto mbaya kwa Uturuki.

Wapiganaji wa kikurdi
Wapiganaji wa kikurdiPicha: Reuters/G. Tomasevic

Mhariri huyo anasema ikiwa Wakurdi wa kaskazini mwa Syria wataungana itakuwa vigumu kwa Uturuki kulizuia vuguvugu la watu hao.Sababu ni kwamba Wakurdi wa Irak nao pia watajiunga, na hapo ndipo linapokuja swali; jee Wakurdi wa Uturuki watafanya nini?

Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" anasema suala la Wakurdi kujitenga halitakubalika kwa Uturuki. Tangu maeneo ya Wakurdi yawe sehemu ya Uturuki ya leo, Uturuki haitakubali hali hiyo ibadilike, na kwa hakika siyo chini ya utawala wa Rais Tayyip Erdogan.

Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anasikitika kwamba dunia inatazama tu, bila ya kuchukua hatua madhubuti nchini Syria, wakati Mamilioni ya watu wa nchi hiyo wanaendelea kuikimbia nchi yao.

Mhariri huyo anaeleza kwamba watu wengi wa nchi hiyo wataendelea kujaribu kukimbilia Ulaya. Lakini bara la Ulaya linajenga kuta ili kuwazuia wakimbizi kuingia. Ni dhihaka ilioje kwamba Uturuki ndiyo inayobeba mzigo mkubwa wa wakimbizi.

Kuhusu mgogoro wa Syria hakuna anaeweza kusema kwamba hana hatia.

Mhariri wa gazeti la "Die Rheinpfalz" anazungumzia juu ya mkataba wa baishara huru baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anasema baada ya Makamu wa Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel kutamka kwamba mazungumzo juu ya kuuleta mkataba huo yamekwama,sasa asishangae kuona kwamba watu wanamsakama na kauli mbaya pia kutoka ndani ya serikali. Labda anacho kifua cha kuzihimihili kauli hizo lakini hatimaye yeye ndiye atakaotoka patupu!

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Iddi Ssessanga