Maoni ya Bernd Riegert juu ya kuupanua Umoja wa Ulaya. | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maoni ya Bernd Riegert juu ya kuupanua Umoja wa Ulaya.

Jee nchi zote zinazowania uanachama wa Umoja wa Ulaya zichukuliwe kwa mpigo au kila moja peke yake ?

default

Iceland pia inawania kuingia katika Umoja wa Ulaya.


Umoja wa Ulaya unakabiliwa na mtihani katika sera yake juu ya kuupanua umoja huo. Wanachama wamegawanyika juu ya suala hilo. Mwandishi wetu, Bernd Riegert, anatoa maoni yake.

Wanachama wa Umoja huo wamegawanyika kati ya wale wanaounga mkono kuingizwa wanachama wapya mara moja na wale wanaoshauri kwenda polepole katika mchakato huo.

Hiyo ni bahati mbaya kwa zile nchi zenye uwezo na zinazotaka kujiunga na Umoja huo. Jee nchi hizo ziingizwe kila mmoja peke yake au ziingizwe zote kwa pamoja.?

Baada ya kuingizwa Bulgaria na Rumania katika Umoja wa Ulaya, baadhi ya wanachama wanataka pawepo mchekecho. Nchi hizo zinanasema wanaostahili kuingizwa katika Umoja wa Ulaya ni wale tu wanaotimiza viwango vyote vilivyowekwa kwenye mkutano muhimu wa viongozi wa Ulaya uliofanyika mjini Copenhagen mnamo mwaka 1993.

Bulgaria na Rumania zilikubaliwa kuingia katika Umoja wa Ulaya miaka miwili iliyopita kwa sababu za kisiasa, ingawa ilifahamika fika kwamba palikuwa na kasoro kubwa katika idara za sheria za nchi hizo na katika harakati za kupambana na rushwa. Na kwa mujibu wa ripoti ya tume ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa hivi karibuni, kasoro hizo bado zipo. Kroatia ambayo imepevuka vya kutosha kuweza kuingia katika Umoja wa Ulaya ilikataliwa kutokana na mgogoro wake wa mpaka na Slovania, mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Mgogoro huo ulizuia mazungumzo juu ya Kroatia kuingizwa katika Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, Kroatia imesema kwa haki kabisa kwamba inatimiza masharti ya kuingia katika Umoja wa Ulaya vizuri zaidi kuliko Rumania na Bulgaria.

Pana tatizo lililojitokeza kuhusu nchi za Yugoslavia ya zamani, zinazotaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Nchi hizo bado zina tofauti za tokea zamani. Yawezekana, kwa mfano, Kroatia, ikiwa mwanachama, ikapinga maombi ya Serbia. Au huenda Montenegro ikapinga maombi ya uanachama wa Serbia. Kutokana na nchi hizo za Yugoslavia ya zamani kuwa na matataizo kati yao, pana swali muhimu la kimsingi la kuuliza; jee kila nchi iingizwe katika Umoja wa Ulaya peke yake au zote zichukuliwe kwa mpigo, na hivyo kuepusha njama za nchi fulani kuitibulia nyingine. Hakuna mwenye jibu kwa sasa kutoka Brussels. Kwa sasa kila mwanachama anajificha nyuma ya mkataba wa Lisbon. Kwa sababu, bado haujaidhinishwa, haitawezekana kuwaingiza wanachama wapya katika Umoja wa Ulaya. Mkataba wa hapo awali- mkataba wa Nizza- ulitoa nafasi kwa wanachama 27 tu. Iwapo mkataba wa Lisbon utapitishwa na nchi zote na kuanza kutumika, Kroatia itaweza kuwa na matumaini. Maombi ya Iceland pia yatazingatiwa kwa makini sana.

Iceland inataka kuingia katika Umoja wa Ulaya kwa sababu za kiuchumi. Hata hivyo, Iceland inatimiza masharti mengi ya kuingia katika Umoja wa Ulaya. Lakini haitakuwa haraka kama jinsi serikali ya nchi hiyo inavyotumai. Lakini wakati ni huu wa kujadili kwa moyo wa dhati juu ya kuupanua Umoja wa Ulaya.


Mwandishi/Riegert Bernd/Mtullya, A.

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 24.07.2009
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/IweC
 • Tarehe 24.07.2009
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/IweC

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com