1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Marekani inachochea mgawanyiko Ulaya

Yusra Buwayhid
5 Juni 2018

Balozi mpya wa Marekani kwa Ujerumani, Richard Grenell amejitumbukiza katika siasa za ndani za Ulaya na kuzua kashfa. Ni tabia isiyo ya kawaida anasema Mkurugenzi Mkuu wa DW Ines Pohl katika uhariri wake.

https://p.dw.com/p/2ywjb
USA New York - Richard Grenell am Trump Tower
Picha: picture-alliance/AP/R. Drew

Ujerumani imekasirishwa. Masaa machache baada ya tovuti ya habari inayoelemea siasa za mrengo wa kulia ya Breitbart kuweka mahojiano iliyofanya na balozi huyo mpya wa Kimarekani kwa Ujerumani. Kuna wanaotaka Richard Grenell, afukuzwe kazi.

Katika mahojiano hayo, balozi huyo aliyeteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump ameeleza nia yake ya kuyawezesha mavuguvugu yanayopinga utawala wa barani Ulaya.

Vipengele vyake vingi katika mahojiano hayo vitawafurahisha wanachama wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia - maarufu kama chama mbadala kwa Ujerumani (AfD), ikiwa ni pamoja na kugusia suala la wananchi wengi wasio na sauti, ruzuku ya serikali kwa wafanyakazi wa kiwango cha wastani, pamoja na wale wanaokosoa sera za Ujerumani kuhusu wakimbizi na kuwaeleza wanasiasa wa Ujerumani kuwa wamepitwa na wakati.

Sio mara ya kwanza kwa Grenell kuingilia mambo ya ndani ya Ujerumani. Muda mfupi baada ya kuteuliwa, aliitaka Ujerumani isistishe biashara na Iran kutokana na mzozo unaoendelea kuhusu makubaliano ya kinyuklia na Iran.

Ines Pohl Kommentarbild App
Mkuu wa Shirika la Habari la Kimataifa la DW, Ines PohlPicha: DW/P. Böll

Si kitu cha kawaida kwa balozi kuingilia mambo ya mwenyeji wake

Ni kitu kisicho cha kawaida kwa balozi kuingilia mambo ya ndani ya mwenyeji wake. Ilivyozoeleka, wadhifa huo unatumiwa kujenga mahusiano ya kidiplomasia na kusuluhisha migogoro. Lakini wale ambao wameshangazwa na tabia za Grenell bado hawakuelewa kwamba, kwa vile Trump yuko ikulu ya Marekani ya White House, kila kitu - ikiwamo diplomasia - kimebadilika.

Trump ni mfanyabiashara, na mafanikio yake makubwa ameyapata katika sekta ya burudani. Uwelewa wake wa siasa hauhusiani kabisa na kile alichokifafanua baba wa muungano wa Ujerumani, Otto Bismarck kama "sanaa ya uwezekano."

Kama ilivyo kwa wale wote wanaounga mkono siasa za kizalendo, Trump na timu yake wanashughulishwa zaidi na kile ambacho kitawapa umaarufu zaidi. Grenell anajua kabisa anachokifanya anapotaja suala la uhamiaji na kumsifu kansela wa Austria wa siasa kali za kihafidhina, Sebastian Kurz. Anataka kuwahamasisha wale walioko Ulaya, ambao kama Trump, wanapingana na hali iliyopo, hasa kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa.

Katika mahojiano hayo, alikuwa akizilenga serikali za kizalendo za siasa za mrengo wa kulia za barani Ulaya, kama zile zilizipo nchini Poland na Hungary, zinazokosoa hali ilivyo kwa sasa barani Ulaya. Zikijaribu kuudhoofisha Umoja wa Ulaya.

Grenell, kama alivyo bosi wake, anatumia hofu za watu kuendeleza ajenga yake. Anaweka shinikizo palipo na udhaifu katika mfumo wa Ulaya ili kuleta mfumo mpya ambao utaudhoofisha Umoja wa Ulaya ili Marekani ifaidike.

Ujerumani na nchi za Ulaya hazina jinsi, bali kukubali kwamba haziwezi tena kuitegemea Marekani. Badala yake, lazima wakubali kwamba Rais wa Marekani anatishia vita vya biashara, na anamtumia mmoja wa wanadiplomasia wake mwenye ushawishi mkubwa barani Ulaya kuleta mgawanyiko katika bara hilo.

Suluhu ni moja tu katika uhusiano huu mpya kati ya Marekani na bara la Ulaya: makubaliano yanayoonyesha mtazamo wa mbali wa kisiasa ulio wazi wa mustakbali wa Umoja wa Ulaya.

Tahariri: Ines Pohl

Tafsiri: Yusra Buwayhid

Mhariri: Josephat Charo