1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano yafikiwa juu ya kupambana na ongezeko la ujoto duniani

7 Juni 2007

Viongozi wan chi tajiri kiviwanda duniani G8 wanaokutana mjini Heilligendamm wamefikia makubaliano ya kupunguza utoaji wa gesi ya sumu inayotoka viwandani kufikia mwaka 2050.

https://p.dw.com/p/CB3i
Viongozi wa G8 wakubaliana kwa kauli moja kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa
Viongozi wa G8 wakubaliana kwa kauli moja kupambana na mabadiliko ya hali ya hewaPicha: AP

Hata hivyo viongozi wa G8 hawajaonyesha kukubaliana juu ya kuwekwa kiwango maalum cha kupunguza gesi za viwandani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anayeongoza mkutano huo wa G8 amewaambia waandishi wa habari kwamba wamekubaliana kwa kimsingi kwanza kukomesha utoaji wa gesi yenye sumu inayotoka viwandani ambayo inasababisha ongezeko la ujoto duniani halafu baadae watazungumzia kuhusu kwa kiwango gani gesi hiyo ipunguzwe.

Hata hivyo ameongeza kusema nchi za G8 zimekubali kufikiria pendekezo lake la kuzitaka nchi zipunguze kwa asilimia 50 moshi wa viwandani ifikapo mwaka 2050 lakini viongozi hao hawajaonyesha nia ya kukubalina na hilo.

Makubaliano yaliyofikiwa ni ushindi mkubwa kwa Kansela Angela Merkel ambaye amasema ameridhishwa na maafikiano hayo.

Muafaka wa leo umefungua njia yakufikiwa makubaliano dhabiti katika mkutano wa Umoja wa mataifa huko Bali Indonesia mnamo mwezi Desemba ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yatakayochukua nafasi ya mkataba wa Kyoto unaomalizika mwaka 2012.

Awali waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair alisema mkutano huu wa kilele wa G8 unaweza kumalizika kwa ahadi za kila upande kupunguza kwa kiwango kikubwa utoaji wa gesi za sumu za viwandani ifikiapo mwaka 2050.

Rais Gorge W Bush wa Marekani ambaye nchi yake inaongoza kwa uchafuzi wa mazingira ambaye amezindua mpango wake mwenyewe wa kufanya mazungumzo na nchi 15 zinazochafua zaidi mazingira juu ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa amesema ni mapema mno kuweka kiwango maalum cha kupunguza gesi hiyo.

Marekani ni nchi pekee katika nchi za kundi la G8 ambayo haijatia saini makubaliano ya Kyoto inayomalizika muda wake mwaka 2012.

Kansela Angela Merkel anatia msukumo katika suala la kuwepo kima maalum cha asilimia 50 cha kupunguza utoaji wa gesi za viwandani kufikia mwaka 2050.

Pendekezo hilo linapingwa vikali na rais Bush lakini wanamazingira wamemuandikia barua bibi Merkal ya kumtolea mwito kuzuia shinikizo za Marekani.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kwa upande mwingine amesisitiza katika mkutano wa leo kwamba lazima paweko viwango maalum vya kupunguza utoaji wa gesi za viwandani kwa kila nchi. Sarkozy ameongeza kusema Marekani inapasa kuzingatia hilo na hakuna atakayeweza kusubiri zaidi kuhusu hilo.

Rais Bush amesema nchi yake iko tayari kuchukua jukumu la kuongoza dunia katika kupamabana na mabadiliko ya hali ya hewa lakini China na India nazo lazima zishirikishwe katika juhudi hizo.

Amesema hakuna kitakachoweza kufanyika linapokuja suala la kupunguza utoaji wa gesi ya viwandani ikiwa China na India hazitashiriki.

Rais Bush pia amepinga shutuma zinazotolewa kwamba Marekani haifanyi lolote kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa akisema utoaji wa gesi za viwandani nchini Marekani umepungua katika kipindi cha mwaka mmoja licha ya kukua kwa uchumi wake.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amezitaka nchi za G8 kulenga kuwa na mtazamo sawa katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.