1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makabila ya kiasili na ardhi zao hatarini

4 Mei 2008

Mahitaji makubwa ya mataifa tajiri duniani,ya nishati inayotokana na mazao ya kilimo,yanahatarisha maisha ya makabila ya kiasili na huteketeza ardhi na misitu ya watu hao.

https://p.dw.com/p/DtCf

Hizo ni hofu zilizoelezwa na wakuu wa makabila ya kienyeji katika mkutano wa kimataifa uliomalizika hivi karibuni mjini New York.Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya makabila ya kiasili,Bibi Victoria Tauli-Corpuz,vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu,kuhamishwa kwa makundi ya watu na migogoro,ni mambo yanayozidi kushuhudiwa.Anasema, sababu kuu ni upokonyaji wa ardhi za makabila ya kiasili pamoja na misitu inayofanywa kuwa mashamba ya mazao yanayotumiwa kutengeneza mafuta ya kuendeshea magari.

Ripoti mpya iliyotolewa kuhusu tatizo hilo inaonya kuwa hadi wenyeji milioni 60 watapoteza ardhi zao na njia za kuendesha maisha yao,ikiwa mahitaji ya mafuta yanayotokana na mazao ya chakula yataendelea kwa kasi ya hivi sasa.Onyo hilo limetolewa wakati ulimwenguni kuna wasiwasi mkubwa kuhusu mzozo wa chakula wa hivi sasa huku mamilioni ya watu duniani,wakikabiliwa na njaa katika maeneo ya kusini.

Wataalamu wa uchumi wa kilimo wanasema,mipango mipya inayotumia vyakula kama vile ngano,mahindi na kadhalika kuzalisha mafuta,ndio iliyosababisha uhaba wa chakula na tatizo kubwa la ongezeko la bei za vyakula kote duniani.Kwa maoni ya wataalamu hao,mzozo huo hautomalizika ikiwa mataifa tajiri hayatobadilisha mfumo wa matumizi yao ya nishati.Kwa mfano Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Sera za Vyakula,inasema,ikiwa mwaka huu nchi tajiri zitasita kutumia nafaka kuzalisha mafuta,basi hatua hiyo itasaidia kushusha bei ya mahindi kwa kama asilimia 20 na ngano kwa kiasi cha asilimia 10 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Kwa upande mwingine,Rais wa Taasisi ya Sera za Dunia yenye makao yake nchini Marekani,Lester Brown, anaonya kuwa tatizo la chakula litazidi kuwa kubwa ikiwa madola makuu hayatoshirikiana kuutuliza umma na kuzuia kutumia nafaka kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya kuendeshea magari.Si hayo tu bali hata matumizi ovyo ya maji na ardhi pamoja na kutokuwepo uwiano wa kibiashara kati ya mataifa,vile vile ni miongoni mwa mambo yanayochochea mzozo wa chakula unaotukabili hivi sasa.

Mapema mwaka huu,Shirika la Umoja wa Mataifa -WFP linaloshughulikia Mipango ya Chakula Duniani liliyahimiza mataifa tajiri kutoa kiasi ya Dola milioni 500 kusaidia tatizo la uhaba wa chakula-hali iliyosababisha ghasia katika nchi fulani.Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Dunia,hadi nchi 33 hivi sasa zipo katika hatari ya kutumbukia katika machafuko ya kisiasa na migogoro ya ndani inayochochewa na mfumko wa bei za vyakula.