1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya umoja wa Afrika yaendelea kufanya doria Anjouan.

27 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DVew

Mutsamudu, Comoro.

Majeshi ya umoja wa Afrika leo yameendelea kushika doria katika kisiwa cha Anzuan visiwani Comoro baada ya kiongozi muasi Mohammed Bakar kukimbilia katika kisiwa cha Mayotte kinachomilikiwa na Ufaransa, akiuacha mji mkuu chini ya udhibiti wa maafisa wa Comoro.

Kiongozi huyo aliyeondolewa madarakani kanali Mohamed Bakar alikimbia kwa kutumia boti yendayo kasi na kuomba hifadhi katika kisiwa cha Mayotte jana Jumatano , siku moja baada ya ushirikiano wa majeshi ya Comoro na yale ya umoja wa Afrika wengi wa wanajeshi wakiwa ni kutoka Tanzania, walipovamia kisiwa hicho katika juhudi za kuviunganisha tena visiwa vya Comoro.

Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa Comoro Mohamed Bakar Dossar, majeshi hayo ya muungano yanatarajiwa kufanya doria kusini mwa Anzuan.

Umoja wa Afrika ulikubali kuweka wanajeshi watapao 1,500 wakiunga mkono kukivamia kisiwa cha Anzuan hatua iliyoamriwa na rais wa visiwa hivyo Ahmed Abdallah Sambi.