1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

27 Julai 2009

Mada iliyogonga vichwa vya habari inahusika na mkasa wa Waziri wa Afya wa Ujerumani alieibiwa gari lake la kiserikali baada ya kulipeleka gari hilo Hispania alikokuwepo mapumzikoni.

https://p.dw.com/p/Iy5L

Tutaanza na gazeti la MÜNCHNER MERKUR linalosema:

"Waziri wa Afya Ulla Schmidt si mgeni katika uwanja wa kisiasa na anazifahamu sheria zinazohusika na kazi hiyo. Orodha ya vitendo vilivyovuka mipaka ni ndefu mno kama vile matumizi mabaya ya gari la serikali, tikti za ndege au kupokea mialiko ya kula katika hoteli za fahari, ni mambo yaliyopunguza imani kati ya watawala na wale wanaotawaliwa. Ulimwengu mzima ukikabiliwa na mtikisiko wa uchumi na benki na makampuni yakipewa misaada mikubwa ya fedha, wananchi bila shaka wana haki ya kutaraji kuwa pesa zao za kodi zinatumiwa kwa busara."

Gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linasema kuwa kwa sasa bado haijulikani ikiwa waziri Schmidt amekiuka sheria zinazohusika na matumizi ya magari ya kiserikali. Likiendelea linasema:

"Wanasiasa pia hufanya makosa,lakini haiwezekani daima kupunguza huduma za jamii na kuwahimiza raia kuishi kuambatana na uwezo wao, wakati wanasiasa wakitumia kila fursa kufaidika kutokana na kazi zao."

Mada nyingine inayotufuata takriban kila siku inahusika na mafua ya nguruwe. Kwa maoni ya gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN homa hii mpya imetufunza moja yaani:

"Homa ya nguruwe inasambaa kwa haraka kila pembe ya dunia. Virusi vyake vinasambazwa kwa kasi na wasafiri wa ndege katika muda mfupi kabisa - kwa hivyo serikali na madaktari vile vile wanapaswa kuchukua hatua za haraka."

Gazeti la BILD ZEITUNG limeshughulikia uchaguzi ujao nchini Ujerumani na limeandika hivi:

"Bado zimebaki siku 62 kabla ya Wajerumani kwenda kupiga kura katika uchaguzi mkuu. Lakini wachunguzi wa maoni kwa kauli moja, wanasema kuwa vyama vya CDU/CSU na FDP pamoja, vitajinyakulia asilimia 50 ya kura zitakazopigwa huku chama cha SPD kikijikokota kati ya asilimia 24 na 26."

Likiendelea linauliza:

"Je, uamuzi umeshapitishwa? Ikiwa ni hivyo basi waliotoa tarakimu hizo wamefanya hivyo bila ya kuwazingatia wale walio muhimu kabisa kupitisha uamuzi, nao ni wapiga kura. Lakini wengi wao mpaka sasa hawakuamua ni chama gani watakachokipigia kura hapo Septemba 27. Kwa hivyo, matokeo ya uchunguzi wa maoni ya leo, hayasemi chochote kuhusu matokeo ya uchaguzi ambao bado haujafanywa."

Gazeti la RHEINZEITUNG likishughulikia tatizo la wale wanaosafiri kwa treni bila ya kununua tikti linasema:

"Wakati huu mgumu ambapo mifuko haina pesa, watu wengi labda hujaribu kusafiri bila ya kununua tikti,kwa hivyo ukaguzi mkali zaidi ni jawabu sahihi. Lakini hapo hapo, shirika la treni lijiulize ikiwa halina lawama. Kwani si kila msafiri anaetaka kuibia. Kwa sehemu kubwa, tatizo hilo linasababishwa na ule mfumo wa bei za tikti unaotatanisha, matatizo ya huduma za shirika hilo la treni na sera zake za kupunguza wafanyakazi. Kwa hivyo, wasafiri hata bila ya kutaka kuibia, hupanda treni bila ya kuwahi kujikatia tikti ya usafiri."

Mwandishi:Prema Martin / DPA

Mhariri:M.Abdul-Rahman