1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

P.Martin9 Juni 2008

Kuongezeka kwa bei ya mafuta na kinyanganyiro cha Kombe la Kandanda la Ubingwa wa Ulaya ni mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya leo huku Ujerumani.

https://p.dw.com/p/EGB5
Germany's Lukas Podolski reacts after scoring his second goal during the group B match between Germany and Poland in Klagenfurt, Austria, Sunday, June 8, 2008, at the Euro 2008 European Soccer Championships in Austria and Switzerland. (AP Photo/Martin Meissner)
Lukas Podolski wa timu ya taifa ya Ujerumani baada ya kuikandika Poland bao la pili,Ujerumani ilipopambana na Poland Juni 8,2008 mjini Klagenfurt,Austria.Picha: AP

Lakini tutaanza na kinyanganyiro kingine kilichowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani:- kampeni ya kuwania kuteuliwa mgombea urais nchini Marekani.

Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linasema:

Kampeni ya Hillary Clinton imemalizika.Seneta huyo ametamka kuwa anaiunga mkono kikamilifu kampeni ya Barack Obama. Mkutanoni alitoa wito kwa wafuasi wake pia kufanya hivyo hivyo baada ya kutangaza kuwa yeye hayupo tena katika kinyanganyiro hicho.

Lakini kwa maoni ya THÜRINGER ALLGEMEINE,mkutano mmoja hautotosha kuwasadikisha wafuasi milioni 18 wa Clinton kumuunga mkono Barack Obama.Wito wa Seneta Clinton ni hatua ya mwanzo na iliyo muhimu kuwashawishi wafuasi wake.Likiendelea linasema,katika wiki zijazo ni vitendo vyake vitakavyoamua umoja wa chama cha Demokratik katika kampeni ya uchaguzi mkuu.

Tukipindukia mada inayohusika na kuongezeka kwa bei ya mafuta kote duniani,gazeti la HEILBRONNER STIMME linasema:

Kuongezeka kwa bei ya nishati kunahatarisha uchumi duniani.Ni dhahiri kuwa kitisho cha kuongezeka kwa bei ya gesi hadi asilimia 40 kutasababisha uchumi kudorora na hasa huku Ujerumani ambako uchumi ulikuwa ukiinukia.

Kwa upande mwingine,gazeti la NORDWEST-ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linauliza:

Je,kwa muda gani serikali ya Ujerumani itaweza kubakia kimya na kutazama yanayotokea katika masoko ya dunia bila ya kuchukua hatua?Labda Korea ya Kusini ina jawabu kwani imeamua kuwapunguzia mzigo wa ongezeko la bei ya nishati hasa wale walioathirika vibaya zaidi.Kwa maoni ya NORDWEST-ZEITUNG ongezeko jingine la asilimia 40 kwa gesi ni jambo lisiloweza kukubaliwa.

Sasa ndio tunageukia mada itakayoendelea kugonga vichwa vya habari magazetini:-kandanda na kombe la ubingwa wa Ulaya.Gazeti la NORD-BAYERISCHER KURIER linasema:

Ukurasa wa kwanza wa hadithi ya mwaka 2008 umeshaandikwa.Ujerumani imejinyakulia ushindi katika mchezo wake wa mwanzo kuwania ubingwa wa kandanda barani Ulaya. Lakini,ushindi huo haumaanishi kuwa Ujerumani itanyakua Kombe la Ubingwa lamalizia NORD BAYERISHER KURIER.