1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri mimea

Josephat Charo7 Novemba 2007

Hali ya hewa inabadilika na hata nchini Ujerumani wataalamu wana hakika kutatokea hali mbaya ya hewa. Taasisi moja ya hapa Ujerumani inajaribu kuvumbua mimea itakayoweza kukabiliana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/C7rL
Mtafiti akichunguza mmea wa mahindi
Mtafiti akichunguza mmea wa mahindiPicha: AP

Hata ikiwa viwango vya joto vinaongezeka, haina maana kuwa miaka 50 ijayo kutakuwa na baridi kali. Michungwa, milimau na mizabibu haitaweza kukuzwa tena katika eneo la kaskazini mwa Ulaya katika siku za usoni. Je ni mimea gani ambayo wakulima wa Ujerumani wanaweza bado kuendelea kuipanda? Shayiri, mahindi, mtama na ngano ni mimea inayoathiriwa sana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea. Wanasayansi tayari wamethibitisha hayo katika uchunguzi wao.

Hali ya baadaye ya kilimo cha eneo la katikati mwa bara la Ulaya itaamuliwa katika eneo linalopatikana kilomita 50 mashariki mwa mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, kandoni mwa barabara inayopitia mashambani. Katika jumba moja kuna mimea midogo inayokua katika mazingira ya baridi. Kinachoweza kuonekana ni makasha ya rangi ya majivu yenye urefu wa karibu mita moja. Kwa Karl-Otto Wenkel, profesa katika taasisi ya Leibniz ya utafiti wa kilimo mjini Müncheberg, makasha hayo yana maana muhimu sana.

´Na ndani ya makasha haya kuna mfumo uliojengwa takriban mita tatu hadi tano ardhini na hapa tunapima mara kwa mara katika mwaka mzima vipi joto la ardhini linavyobadilika na vitu vingapi kutoka sehemu fulani ya ardhi vinadidimia ardhini na vinakwama wapi. Vitu gani vilivyoyeyuka ndani ya maji ambavyo vinaingia katika maji yaliyo chini ya ardhi. Kiasi gani cha gesi ya naitrojeni kilicho ndani na kinaathirika vipi baada ya shughuli za kilimo.´

Utafiti unaofanywa katika mashamba unatakiwa kuwa ufunguo wa kuvumbua mifumo mipya ya kilimo na njia mpya za kunyunyizia mbolea. Hilo ni jiwe la msingi katika mfululizo wa utafiti unaotakiwa kupima na kudhihirisha athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika kilimo. Ushahidi zaidi wa utafiti huo unapatikana katika nyumba mnamokuzwa mimea katika taasisi ya Leibniz kama anavyoeleza profesa Karl-Otto Wenkel.

´Kwa hiyo upande wa kushoto kuna jengo ambalo ndani lina vyumba vyenye hali mbalimbali ya hewa. Vyumba hivi vina faida moja kwamba ninaweza kuwasha taa na kubonyeza kifungo cha joto wakati mmoja. Na huo ni msingi wa uchunguzi wa kutafuta vipi mimea iliyo katika joto linalobadilika badilika na mwangaza, inavyokua na kufanya kazi.´

Profesa Karl-Otto Wenkel amesema ni lazima kuchunguza vipi mimea inavyoathiriwa na joto jingi, mwangaza mwingi wa jua na juu ya yote na kiwango cha gesi ya carbon dioxide kupita kiasi cha kawaida kinachohitajika kwa mimea. Kwa hiyo taasisi ya Leibniz imeshirikiana na taasisi moja mjini Braunschweig kufanya uchunguzi kwa kuiweka mimea ya nafaka katika mazingira yenye gesi nyingi ya carbon dioxide. Matokeo ya mwanzo yameonyesha ufanisi. Mimea ya shayiri na ngano inakuwa vizuri zaidi kuliko kawaida.

Hata hivyo profesa Wenkel anaonya kwamba kuna hatari inayoweza kutokea, ´Lakini kunaweza kutokea hatari nayo ni kuharibika kwa ubora wa maganda na kwa ghafla. Ubora wa maganda na wingi wa protini unapungua na kwa sasa hatujui hilo lionasababishwa na nini. Kunapokuwa na nitrojini nyingi, ubora wa maganda unakosekana ikiwa kuna kiwango kikubwa cha gesi ya carbon dioxide. Na sasa lazima tuchunguze ni hatua gani zilizopo za kurekebisha hali hiyo. Je majimaji yanaweza kufanya lolote au ni kitu gani kinachotakiwa kubadilsishwa ili kuzuia mwenendo huu mbaya.´

Kinachotakiwa hasa kufanywa na binadamu ili kuhakikisha mikate, piza na keki zitaokwa miaka hamsini ijayo, ni jambo linalomshughulisha sana profesa Karl Otto Wenkel. Amejitolea kwa dhati kufanya uchunguzi utakaovumbua mimea itakayoweza kumudu mabadiliko ya hali ya hewa.