1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto kwa viongozi wa G8

Saumu Mwasimba7 Juni 2007

Viongozi wa nchi 8 tajiri kabisa kiviwanda duniani G8 wanaendelea na mazungumzo yao yalioanza rasmi hii leo.

https://p.dw.com/p/CB3j
Viongozi waliohudhuria mkutano wa G8 Ujerumani
Viongozi waliohudhuria mkutano wa G8 UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Kikao cha leo kinafanyika huku kukiwa na mgawanyiko juu ya kulitatua suala la mabadiliko ya hali ya hewa na mvutano wa mahusiano kati ya Urussi na nchi za Magharibi.

Mkutano wa kilele wa kundi la G8 ukiongozwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel huenda leo hii ukagubikwa na mjadala mkali kuhusu suala la kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa huku rais wa Marekani akiendelea kuyapinga mapendekezo ya kansela Angela Merkel ya kuzitaka nchi za G8 zijitolee kikamilifu kupunguza kwa asilimia 50 utoaji wa gesi za sumu kutoka viwandani zinazoongeza kiwango cha joto duniani ifikiapo mwaka 2050 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1990.

Kansela Merkel pia anazitaka nchi hizo kuongeza matumizi ya nishati mbadala zisizochafua mazingira kwa asilimia 20 ili kupunguza kiwango cha joto katika karne hii kwa nyuzi 2 za Celsius.

Kamishna wa tume ya Ulaya ambaye pia anashiriki kikao cha G8 amewaambia waandishi wa habari kabla ya kuanza kikao cha leo kwamba kufanikiwa au kushindwa kwa kikao cha leo kutategemea ikiwa viongozi wanaokutana watakubaliana na malengo kama hayo yaliyotolewa na Merkel na kukubali wazo la kuwa na mazungumzo zaidi na Umoja wa mataifa juu ya suala hilo la mabadiliko ya hali ya hewa.

Hapo jana rais Bush ambaye nchi yake ni mchafuzi mkubwa wa mazingira alisisitiza kwamba anataka sana kushirikiana na bibi Merkel katika suala hilo la kupunguza gesi za sumu zitokazo viwandani hasa kutokana na kwamba muda wa rasimu ya Kyoto unamalizika mwaka 2012.

Hata hivyo rais Bush hakuonyesha dalili yoyote ya kulainisha msimamo wake panapokuja suala la kuwekwa kiwango maalum cha kupunguza utoaji wa gesi hiyo.

Marekani imesema inapendelea zaidi kupunguza utoaji wa gesi za viwandani kupitia technologia mpya na inataka hatua za ushirikiano juu ya suala hilo na nchi zinazochafua mazingira zaidi zikiwemo China na India.

Mshirika wa karibu war ais Bush katika masuala mengi Tony Blair pia amesema huenda viongozi wakakubaliana wiki hii katika kupunguza utoaji wa gesi za sumu za viwandani lakini hawataweka kima maalum cha upunguzaji wa gesi hiyo.Wakati huo huo kabla ya kuanza kikao cha leo rais Bush ameitolea mwito Urussi isiingiwe na wahka juu ya mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya ulinzi katika ulaya ya mashariki.

Matamshi hayo ya Bush ameyatoa kabla ya kukutana na rais Vladmir Putin ambapo mazungumzo yao yanatarajiwa kugubika kikao cha mwanzo cha siku nzima kwenye mkutano wa G8.Urussi inaamini kuwa ni mlengwa wa mfumo huo wa makombora ya marekani na rais Putin ametishia kuyaelekeza makombora hayo katika nchi za ulaya ikiwa yatawekwa.

Masuala mengine yanayotazamiwa kuzungumziwa na viongozi wa G8 ni pamoja na hatma ya jimbo la Kosovo, hali ya mambo katika mashariki ya kati pamoja na juhudi za kimtaifa za kuishwishi Iran ikubali kusimamisha urutubishaji wa madini yake ya Uranium.