1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwanini Ujerumani imelengwa na magaidi?

1 Desemba 2015

Kwa muda mrefu idara za usalama za Ujerumani zimehofia kutokea mashambulio ya kigaidi, hasa kutokana na sera ya nje ya Ujerumani. Lakini sababu siyo tu kuhusika kwa Ujerumani huko Iraq na Afghanistan.

https://p.dw.com/p/1HFGO
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere
Picha: Reuters

Baada ya mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11 mwezi Septemba nchini Marekani, ni swali moja tu ambalo limekuwa linaulizwa wakati wote katika vyombo vya habari vya nchi hiyo. Kwanini wanatuchukia?

Baada ya mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11 mwezi Septemba nchini Marekani, ni swali moja tu ambalo limekuwa linaulizwa wakati wote katika vyombo vya habari vya nchi hiyo. Kwa nini wanatuchukia? Hali ni tofauti nchini Ujerumani: Idara za usalama na wananchi kwa jumla wanajua tangu muda mrefu kwamba nchi yao inaweza kushambuliwa na magadi wakati wowote. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, wakati wote amekuwa anatahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea hatari hiyo.

Mtaalamu kutoka chuo cha Milan cha mitaala ya siasa za kimataifa, Lorenzo Vidino, anaona kwamba sababu kubwa inaweza kuwa sera ya nje ya Ujerumani. Mtaalamu huyo amefafanua kwamba tangu Ujerumani ishiriki kijeshi nchini Afghanistan, wanajihadi wanaiona Ujerumani kuwa sehemu ya harakati zinaoongozwa na Marekani katika kuupiga vita Uislamu. Hatari ya Ujerumani kushambuliwa na magaidi imezidi kuwa kubwa tangu serikali ya nchi hii ianze kushiriki katika juhudi za kupambana na magaidi wa "Dola la Kiislamu - IS."

Mashambulio ya kigaidi Marekani, tarehe 11 Septemba 2001
Mashambulio ya kigaidi Marekani, tarehe 11 Septemba 2001Picha: AP

Mtaalamu wa Ujerumani wa masuala ya ugaidi Rolf Tophoven, amesema Ujerumani inaweza kushambuliwa wakati wowote kwa sababu magaidi wanaiona Ujerumani kuwa sehemu ya jumuiya ya magharibi.

Tophoven ameeleza kwamba Ujerumani imekuwa inalengwa na waislamu wenye itikadi kali tangu ianze kuwapelekea silaha, na kuwapa mafunzo wapiganaji wa kikurdi wa Pershmega wa kaskazini mwa Iraq, wanaopambana na magaidi wa Dola la Kiislamu.

Dola la Kiislamu limesambaa kote

Hata hivyo, sera ya nje siyo sababu ya pekee inayoweza kufanya Ujerumani ishambuliwe na magaidi. Mtaalamu wa masuala ya kimataifa kutoka chuo cha Milan ametahadharisha kuwa hata nchi ambazo hazimo katika mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magaidi kama Sweden na Uswisi mipango ya kufanya mashambulio ya kigaidi iliwahi kuzuiwa. Mtalamu huyo ameeleza kuwa hali hiyo inatokana na mnyumbuko uliopo muundo wa magaidi.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen, atembelea majeshi ya Ujerumani huko Afghanistan
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen, atembelea majeshi ya Ujerumani huko AfghanistanPicha: Reuters/J MacDougall

Kundi la magaidi hao linatokana na watu mbalimbal binafsi, wenye mashikamano ya ndani na makundi kama vile ya al-Nusra, al-KQaeda au hata Dola la Kiislamu. Mtaalamu huyo ameeleza kwamba watu hao wapo huru kuchukua hatua zao. Bwana Vidivo amesema ikiwa, mathalani, watu hao wanaishi nchini Sweden na wanaendesha harakati, kiitikadi au kimapambano, wanafanya hivyo chini ya kaulimbiu inayosema, fikiria kimataifa lakini chukua hatua pale ulipo.

Kwa wanaoitwa wanajihadi waliozaliwa na kukulia katika nchi za magharibi, mambo ya ndani ya nchi zao, kama vile hisia za kubaguliwa yanaweza kuwa sababu ya kufanya ugaidi. Lakini pia sera za nje zinaweza kuwa sababu.

Asiem El Difraoui mwenye ufahamu wa undani juu ya propaganda ya waislamu wenye itikadi kali anakumbusha kwamba kufanya mashambulio dhidi ya nchi za magharibi, tangu muda mrefu ni sehemu thabiti ya itikadi ya watu hao. Hata hivyo ameeleza kwamba magaidi wa "Dola la Kiislamu" wamechapuka kidogo nje ya mkakati huo, kwa sababu wafuasi wao walizielekeza nguvu zao katika ujenzi wa nchi ya Kiislamu nchini Syria na Iraq.

Ndiyo sababu kwa sababu za kimikakati wamesema hawatazishambulia nchi za magharibi kwa matumaini ya kuepuka kushambuliwa. Lakini baada ya Marekani kuanza kuzishambulia ngome zao, magaidi wa Dola la Kiislamu waliubadilisha mkakati wao. Tangu kuanza mashambulio ya ndege dhidi yao, magaidi hao wameeleza wazi kwamba nchi zote za magharibi zinaweza kushambuliwa.

Nia ni kugawanya watu

Mtaalamu Asiem El Difraoui amesema mashambilio ya magaidi hao yanalenga shabaha mbili, kwanza ni kushinikiza: Magaidi hao wametambua kwamba baada ya mji mkuu wa Uhispania, Madrid kushambuliwa na magaidi mnamo mwaka wa 2004, Uhispania iliyaondoa majeshi yake kutoka Iraq. Watu wapatao 200 waliuawa kutokana na shambulio hilo. Lengo la pili ni kuzigawanya jamii za magharibi.

Mazishi ya wahanga wa shambulio la Madrid 2004
Mazishi ya wahanga wa shambulio la Madrid 2004Picha: picture-alliance/dpa

Lakini matokeo yake ni kuchochea hisia dhidi ya uislamu na mashambulio. Hata hivyo hali hiyo inaweza kuwafanya vijana wa Kiislamu wahisi kutengwa na jamii za walio wengi. Hiyo ni rutuba kwa watu wanaowaghiribu vijana hao ili wajiunge na magaidi.

Mtaalamu Rolf Tophoven amesema sababu kuu ya mashambulio yanayofanywa na magaidi wa Dola la Kiislamu, ni kutoa ujumbe mkubwa zaidi. Kwa kuweza kuvuka mipaka na kuingia Syria na Irak, wapiganaji wa Dola la Kiislamu wamefanikiwa kuwatimua magaidi wengine ambao ni al-Qaeda.

Mwandishi: Dennis Stute

Mfasiri: Abdu Mtullya

Mhariri: Josephat Charo