Kurasa Zilizopotea: Kampeni ya kuwaunganisha Waislamu na Wayahudi | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kurasa Zilizopotea: Kampeni ya kuwaunganisha Waislamu na Wayahudi

Uingereza imezindua kampeni iliyopewa jina la Kurasa Zilizopotea, ambayo inahusiana na Siku ya Kumbukumbu ya Maangamizi ya Mayahudi barani Ulaya, kwa lengo la kuonesha historia ya mshikamano baina ya jamii hizi mbili.

Familia ya Kiyahudi nchini Albania

Familia ya Kiyahudi nchini Albania

Kampeni ya 'Missing Pages', yaani Kurasa Zilizopotea ilizinduliwa na mbunge Muislamu katika bunge la House of Lords, Lord Patel, ambaye anasema kuwa kampeni hii inakusudia kuangazia historia yenye utajiri wa kuishi pamoja na kustahmiliana kati ya Waislamu na Wayahudi.

"Hisia mbaya dhidi ya Mayahudi ni jambo lisilo nafasi kwenye Uislamu. Na tunahitaji kuzifufua kumbukumbu za mashirikiano na kuishi kwa amani kulipokuwepo kati ya jamii hizi." Amesema Lord Patel.

Kampeni hii inaendeshwa na wakfu wa Exploring Islam, ambao unajaribu kujenga uelewa wa watu kuhusu Uislamu na kupingana na dhana potofu dhidi ya Waislamu. Kwa mujibu wa balozi wa dunia wa wakfu huu, Kristiane Backer, ambaye mwenyewe ni mtangazaji wa televisheni wa Kijerumani anayeishi jijini London, Kurasa Zilizopotea inaelezea kwa kiasi kikubwa zile hadithi ambazo hazijawahi kusemwa.

Hadithi iliyosahauliwa

Umoja wa kidini, Uislamu, Ukrisro na Uyahudi

Umoja wa kidini, Uislamu, Ukrisro na Uyahudi

“Kampeni hii inaelezea hadithi zilizosahauliwa za ujasiri, ushujaa na huruma ambao uliweza hata kuhatarisha maisha ya waliokuwa nao wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Ni hadithi za Waislamu na Mayahudi ambazo tunatarajia zitaleta msukumo mwema kwa mustakabali wetu." Anasema Backer.

Kwa ujumla kampeni hii inajikita kwenye kazi ya mpiga mpicha wa Kimarekani mwenye asili ya Kiyahudi, Norman Gershman, ambaye hivi karibuni alitembelea Albania alikokwenda kupiga picha familia za Kiislamu ambazo ziliwaokoa Mayahudi wakati wa Vita Pili vya Dunia. Sehemu moja ya kazi hiyo hivi sasa inatengenezwa kuwa filamu fupi.

Wakati muafaka

Familia ya Kiyahudi mjini Sarajevo

Familia ya Kiyahudi mjini Sarajevo

Picha za Gershman zinaoneshwa katika vyuo vikuu kadhaa nchini Uingereza hivi sasa kama sehemu ya Kampeni ya Kurasa Zilizopotea, kwa ushirikiano wa jumuiya za Kiislamu na Kiyahudi. Gershman mwenyewe anasema kwamba sasa ndio wakati muafaka wa kutoa mwanga kwa hadithi hizi za Albania.

“Unajua kuwa tuna ile kasumba ya jumla-jamala kuwa Waislamu wote ama ni magaidi au wanaunga mkono magaidi. Kama vile kusema kuwa Mayahudi wote ni wakopeshaji fedha au Wakristo wote ni wauaji wa vita vya msalaba. Ni upumbavu. Ni wendazimu kabisa na mimi siwezi kuukubali." Amesema Gershman.

Miongoni mwa watu waliokuwapo kwenye uzinduzi wa kampeni hii ni Dkt. Scarlett Epstein, ambaye mwenyewe ni Myahudi aliyepatiwa hifadhi nchini Albania wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, baada ya nchi nyengine za Ulaya, ikiwemo Uingereza, kukataa kumpokea. Anasema ana deni la milele kwa Waislamu wa Albania:

“Tulikuwa kundi la kiasi Mayahudi 50 kutoka Ujerumani, Poland na Austria na tuliishi kwenye nyumba kama wajima. Tuligawana na kuchangiana kila kitu, tulitengeneza samani zetu wenyewe; tena tukiwa karibu na kituo cha polisi. Na wale polisi wote walikuwa Waislamu. Na kama wakimbizi wote, tulifikiria kuwa ni jambo zuri kuwa marafiki na polisi, kwa sababu viza zetu pia zilimalizika muda kwa kuwa tulikuwa na viza za watalii tu, lakini Waalbania, tafauti na Wayugoslavia, kamwe hawakutaka kutufukuza. Na kwa sababu walikuwa ni Waislamu, walitaka kutusaidia na sio kututendea mambo mabaya." Amesimulia Dkt. Epstein.

Lakini wakati kampeni hii ya kukumbuka Maangamizi dhidi ya Jamii ya Kiyahudi barani Ulaya inajikita kwenye yale mambo mema kati ya Waislamu na Mayahudi, inaonekana kama ni njia ya kupingana na kile baadhi ya washiriki wake wanachosema, ni kukuwa kwa hisia za chuki dhidi ya Mayahudi katika jamii za Waislamu wa Uingereza na pia chuki dhidi ya Waislamu kwa waandishi wa Kiyahudi nchini humo.

Matarajio ni kuwa kiwango hiki kikubwa cha hadithi zilizokuwa hazijawahi kutolewa kutoka Vita vya Pili vya Dunia zitaweza kusaidia katika kuimarisha mahusiano mema baina ya jamii hizi mbili nchini Uingereza.

Mwandishi: Olly Barratt/ZPR/Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/105ZJ
 • Tarehe 27.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/105ZJ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com