KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA | Michezo | DW | 05.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA

Hatimaye timu nne zitakazoumana katika nusufainali ya kombe la afrika, zimekwisha julikana na baada ya Misri na Cameroon kushinda mechi zao hapo katika robofainali ya kukata na shoka.

Nusufainali hizo itawakutanisha Mabingwa watetezi Misri,Ivory Coast, wenyeji Ghana na Cameroon.


Mabao mawili ya Stephen Mbia yaliwasaidia Simba Wanyika Cameroon kuwasukumiza nje Tunisia katika ushindi wa mabao 3-2 jana usiku ambapo mbabe alipatikana katika muda wa nyingeza.


Kocha wa Tunisia Mfaransa Roger Lemmere alikiri kuwa Simba Wanyika walikuwa imara zaidi yao na kwamba ni vigumu kucheza na timu kama hiyo ambayo ina nguvu na stamina.


Kwa upande wake kocha wa Simba hao Wanyika Cameroon Mjerumani Otto Pfister alisisitiza kurejea kwa uwezo wa timu yake kupachika mabao.


Simba hao Wanyika sasa wataumana na wenyeji Ghana katika nusufainali mjini Accra, na mjerumani huyo amesema kuwa jana walipta usingizi mzuri kabla ya maandalizi ya nusufainali hiyo.


Ghana iliingia nusufainali kwa kuifurusha Nigeria mabao 2-1, na sasa inajiwinda kuwatimua Cameroon hiyo keshokutwa.


Nusufainali hiyo inasubiriwa kwa hamu , huku waghana wakijinasibu kushinda mechi hiyo na kwa upande wao Cameroon wakisema kuwa baada ya kuanza vibaya sasa kazi ni moja tu ushindi.


Dr Francis Nuno ambaye ni mkufunzi katika chuo kikuu cha Accra ni miongoni mwa waghana wenye wazimu mkubwa wa soka .


Nusufainali nyingine itakuwa ni marudio ya fainali ya miaka miwili iliyopita nchini Misri, kati ya mabingwa watetezi Misri na Tembo wa Ivory Coast.


Mafarao wa Misri waliyoanza kwa kishindo utetezi wao kwa kuitandika Cameroon mabao 4-2, jana iliwabidi kufanya kazi ya ziada kuifunga Angola mabao 2-1 na sasa wataumana na Ivory Coast siku hiyo hiyo ya alhamisi mjini Kumasi.


Kocha msaidizi wa Misri Shawky Gharib amesema kuwa sasa wanajiwinda kuwakabili Ivory Coast wanaopigiwa upatu na wengi kuweza kushinda kombe hilo.


Ivory Coast watataka kulipiza kisasi cha kunyang´anywa tonge mdomoni mjini Cairo walipofungwa na Misri kwa mikwaju ya penalti katika fainali.


Tembo hao Ivory Coast waliingia nusufainali kwa ushindi mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya Guinea.

 • Tarehe 05.02.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/D2UL
 • Tarehe 05.02.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/D2UL