Kombe la CECAFA -KAGAME CUP lanyakuliwa na APR ya Rwanda. | Michezo | DW | 31.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la CECAFA -KAGAME CUP lanyakuliwa na APR ya Rwanda.

Ujerumani yailaza Hungary mabao 3:0 ikijandaa kwa Kombe la dunia.

default

Samuel Eto'o (kati) amjibu Milla-kafanya nini ?

Kombe la Kagame-kanda ya Afrika Mashariki na Kati- limebakia nyumbani Rwanda baada ya Timu ya Jeshi la Taifa, APR kuilaza St.George ya Ethiopia. Tanzania,homa ya Kombe la dunia,imewapata mashabiki kwa kuwasili Brazil wiki ijayo kwa mpambano na Taifa Stars.Lakini, je, watanzania watamudu ada za kuingia uwanjani hadi Tsh.200.000?

Samuel Eto-o -stadi wa Kameroun, alietamba na FC Barcelona na majuzi na Inter Milan, walipotwaa Kombe la Champions League,auliza simba wa nyika -mzee Roger Milla, yeye kafanya nini hata anamkosoa Eto-o ?

Na mabingwa mara 3 wa dunia-Ujerumani, walioilaza Hungary juzi mabao 3-0,jiinamizi la kuumia mastadi wake, lingali linawaandama:Mchezaji mwengine ameumia -muda mfupi kabla kuelekea Afrika kusini.

KOMBE LA CECAFA:

APR ya Rwanda ni mabingwa wa Kombe la Kagame-kombe la klabu bingwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati baada ya kuilaza St.George ya Ethiopia, katika finali ya mwishoni mwa wiki. Baada ya timu hizo 2 kusimama sare,uamuzi ulikatwa baada ya kurefushwa mchezo.

Wakati Rwanda, washerehekea ushindi wa Kombe la Kagame, lililobaki nyumbani Kigali, mashabiki wa Tanzania,wameandaa Jumatano ijayo-finali yao ya Kombe la dunia kati ya Taifa Stars na mabingwa mara 5 wa dunia, Brazil. Lakini ilistahiki kutumia Shillingi bilioni 1 kuileta Brazil Tanzania ? Je, nani atamudu bei za Tiketi za kiingilo ?

Kuileta Brazil kucheza Tanzania, inasemekana imeiligharimu Shirikisho la dimba la Tanzania-bara TFL kitita cha Tsh.Bilioni 1.S Kiingilio kwa mpambano wa Jumatatu ijayo mjini Dar-es-salaam ni TSH 200.000 kwa VIP A.TSh.150.000 Kwa VIP B hadi Tsh.30.000 ikiwa bei ya chini kabisa.

Mjadala motomoto umezuika Tanzania iwapo ilistahiki kutumia kitita kama hicho kwa kuileta Brazil kwa mpambano 1 ? Kwa upande mwengine, ni mara ya kwanza kwa Brazil kucheza Afrika Mashariki. Mpambano kati ya Brazil na Taifa Stars ni pia wa kujinoa kwa Taifa Stars kwa changamoto yake na Ruanda Jumamosi itakayofuatia mpanbano huo.

Tukibakia katika maandalio ya Kombe lijalo la dunia,nahodha wa Bafana Bafana au Afrika Kusini, Aaron Makoena,atakuwa mchezaji wa kwanza kabisa wa Afrika kusini kuichezea leo timu hiyo ya Taifa mara 100 pale Bafana Bafana, itakapingia uwanjani jioni hii kucheza na Guatammala, mjini Johannesberg.

Stadi huyo mwenye umri wa miaka 29,maarufu kwa jina la "Mbazo"-yaani shoka,beki wa kati ya uwanja, anaeichezea Portsmouth,ya Uingereza.Wiki iliopita, Afrika Kusini, iliikomea Colombia mabao 2:1 ikijiandaa kwa Kombe la dunia.Afrika kusini itafungua dimba Juni 11 kati yake na Mexico.Kwanza lakini, inatumai kutamba tena hii leo dhidi ya Guatamala.

MVUTANO KATI YA ROGER MILLA NA SAMUEL ETO-O:

Mfarakano umeibuka nchini Kameroun, kati ya stadi mzee na mchanga:Mzee Roger Milla,amemtuhumu Samuel Eto-o, kutofanya lolote kwa Kameroun.Roger Milla, aliliambia wiki iliopita shirika la habari la AFP kwamba, Eto-o ameleta mafanikio makubwa kwa FC Barcelona na Inter Milan,lakini hakufanya lolote kwa nchi yake Kameroun.

Akijibu,Samuel Eto-o ,ambae mwezi huu alishinda taji la Champions League na Inter Milan ya Itali na kuongezea mataji kama hayo aliovaa na FC Barcelona ya Spain ,2006 na 2009, alisema Milla aonesha ana uchungu mkubwa. Akauliza: iwapo anastahiki kujiunga na Kameroun kucheza Kombe lijalo la dunia ? Akasema atazingatia swalio hilo siku chache zijazo,kwani, hahitaji kushiriki katika Kombe la dunia kwa maisha yake ya dimba.

Akakumbusha Eto-o kwamba, mara nyingi karibu na mashindano makuu, watu wenye uchungu huonesha hasira zao. Akauiliza,Milla kafanya nini ? Milla hakushinda Kombe la Dunia, ndio walifika robo-finali ya kombe la Dunia 1990 lakini na timu gani ? Aliuliza Eto-o.

Roger Milla,akiwa na umri wa miaka 38 ,alitia mabao 4 katika mechi 5 iliocheza Kameroun,1990 huko Itali na kuingia katika ukumbi wa mastadi mashuhuri wa dimba wa Afrika.

Mabingwa mara 3 wa Dunia-Ujerumani, waliendelea kujiandaa kwa kombe la dunia pale walipoizaba Hungary mabao 3:0 hapo Jumamosi.Ujerumani ilitwaa Kombe la dunia 1954 kwa kuilaza Hungary,ikavaa tena taji nyumbani 1974 na kwa mara ya tatu 1990 nchini Itali ilipoitoa Argentina.

Baada ya kuumia nahodha wake Michael ballack, kipa wa Taifa Rene Adler, juzi ameumia stadi wake mwengine aliekewa matumaini makubwa kwa Kombe la dunia: dakika za mwisho za mpambano na hungary hapo Jumamosi, Heiko Westermann wa Schalke 04.Nae pia sasa amebidi kuliacha jahazi linaloelekea Afrika kusini chini ya usukani wa Philipp Lahm, nahodha mpya.

Westermann alisema:

"Kwangu mimi binafsi na hata kwa timu ya Taifa mambo ni mabaya kwa kuumia ni kama kuumia kwa Ballack na Christian,hali si nzuri.Lakini sifa na nguvu za timu ya Ujerumani ipo pale pale.Nina hakika,hatahivyo, tutacheza Kombe la Dunia kwa mafanikio."Alisema,Heiko Westermann.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 31.05.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/Ne5l
 • Tarehe 31.05.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/Ne5l