Kocha Loew ataja kikosi cha Die Mannschaft
4 Juni 2018Wakati macho na masikio ya wapenzi wa kandanda duniani yanaelekezwa nchini Urusi. Vikosi mbali mbali rasmi vya timu zinazoshiriki katika fainali hizo vinatangazwa leo kwa matayarisho ya mwisho kabla ya michuano hiyo kung'oa nanga hapo Juni 14 siku 10 kuanzia sasa. Ujerumani ikiwa ni mabingwa watetezi wa kombe la dunia imetangaza pia kikosi chake rasmi.
Mchezaji wa kati mshambuliaji kutoka klabu ya Manchester City Leroy Sane atakosekana katika kikosi cha mwisho cha kocha Joachim Loew cha timu ya taifa ya Ujerumani Die Mannschaft kwa ajili ya fainali za kombe la dunia kwa mujibu wa taarifa leo wakati mlinda mlango Manuel Neuer alitajwa miongoni mwa wachezaji 23 wanaokwenda Urusi kutetea ubingwa huo.
Neuer alijumuishwa katika kikosi hicho licha ya kucheza katika mchezo mmoja tu rasmi , mchezo wa kirafiki dhidi ya Austria siku ya Ijumaa, tangu alipovunjika mfupa mdogo wa nyuma wa mguu wake mwezi Septemba mwaka jana lakini mchezaji mwenye kipaji Sane mwenye umri wa miaka 22 ni jina kubwa ambalo halimo katika orodha hiyo.
Mchezaji huyo wa Manchester City, mlinda mlango Bernd Leno, mshambuliaji Nils Petersen na mlinzi Jonathan Tah ni wachezaji wanne ambao wameshindwa kumshawishi kocha Joachim Loew kwamba wanaweza kuisaidia timu hiyo katika fainali za kombe la dunia.
Loew alitangaza kikosi chake mwishoni mwa kambi ya mazowezi katika milima ya Alps nchini Italia. Ujerumani itacheza mchezo wake wa mwisho wa matayarisho dhidi ya saudi arabia mjini Leverkusen siku ya Ijumaa kabla ya kuanza kwa mashindano hayo Juni 14.
Nae kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliwatembelea wachezaji wa timu hiyo ya taifa jana Jumapili na kuzungumza nao juu ya uzoefu wake kuhusu Urusi kabla ya kikosi hicho kutangazwa rasmi leo. Baada ya chakula cha jioni katika hoteli katika jimbo la kusini nchini Italia la Tyrol , Merkel , ambaye huzungumza ugha ya kirusi bila matatizo baada ya kukulia katika iliyokuwa Ujerumani mashariki ya zamani , alikiambia kikosi hicho juu ya nchi hiyo na watu wake, meneja wa timu hiyo Oliver Bierhoff alisema.
"Tumefarijika sana kwamba aliweza kuchukua muda wake na kukutana nasi. Bila shaka ziara ya kansela ni muhimu kila wakati. Na ilikuwa sio ziara rasmi, na alipata fursa ya kuzungumza na wachezaji. Lakini si hayo tu, bali pia kansela anaifahamu vizuri Urusi na alizungumzia kuhusu nchi hiyo na watu wake na pia kuhusu maoni yake kuhusu Urusi na kutufahamisha taarifa za msingi kuhusu nchi hiyo."
Rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani DFB, Reinhard Grindel amesema, kwamba ziara ya masaa matatu ya Merkel ilikuwa ya uwazi na iliyofanikiwa sana. "Alitutakia kila la kheri na bahati njema," aliongeza nahodha msaidizi Sami Khedira. Ilikuwa mkusanyiko wa utulivu kabisa. Kansela ambaye pia alichukua muda kusalimiana na wapenzi wa kandanda nje ya hoteli hakuhusisha vipingamizi vingi, alionesha utu, mkweli na mwenye hamasa sana, alisema Khedira.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe /dpae
Mhariri: Josephat Charo