1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipato duni kigezo cha kupata virusi vya corona

Sudi Mnette
16 Mei 2020

Watafiti wa Uingereza wamebaini kwamba watu wanaoishi katika mazingira duni nchini humo, wapo katika hatari zaidi kupata maambukizi ya COVID-19. Wakati, huko Brazil kumerekodiwa kiwango cha juu cha maambukizi.

https://p.dw.com/p/3cJft
England COVID-19 in London
Picha: Reuters/H. Nicholls

Zaidi ya watu 307,000 wamekufa kwa COVID-19 duniani kote, wakati kumerekodiwa pia maambukizi milioni 4.5. Miji ya Ujerumani inajiandaa kuandamana dhidi ya vizuizi vya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ambapo idadi kubwa ya watu inatarajiwa katika miji ya  Munich, Berlin na Stuttgart.

Kwengineo watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford wamebaini kuwa kiwangio cha kipato ni kigezo muhimu katika kesi za maambukizi, ambapo wale wenye kipato kidogo wapo katika hatari zaidi ya maambukizi. Utafiti huo uliofanywa kwa watu 3,600 ulibaini pia wenye magonjwa sugu wameathiriwa vibaya. Asilimia 29.5 wanaoishi katika mazingira duni walibainika kuwa na virusi ikilinganishwa na asilimia 7.7 ya wanaoishi katika maeneo ya kitajiri. Watu wenye umri wa miaka kati ya 40 na 64 wamebainika kuwa katika hatari zaidi ya asilimia 18.5 ikilinganishwa na kundi la umri wa miaka 17 ambao wapo katika hatari ya asilimia 4.6.

Rais Trump aonesha matumani ya kupatikana kwa chanjo ya virusi vya corona

US Präsident Trump
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/CNP/A. Harrer

Rais Donald Trump wa Marekani amesema serikali yake itawekeza kwa makampuni yote makubwa yanayofanya jitihada za kutafuta chanjo ya virusi vya corona na kwamba imepunguza idadi ya makampuni hayo hadi kufikia 14, huku akitoa ahadi ya kuyapunguza zaidi. Katika mkutano wake uliofanyikia Ikulu ya Marekani, ambapo ulihudhuriwa na maafisa wengi wa Ikulu hiyo wakiwa wamevaa barakoa, lakini yeye akiwa hajavaa, Trump alionesha matumaiini kwamba kinga ya maradhi ya COVID-19 kabla ya kumalizika mwaka huu.

Waziri wa Afya wa Brazil Nelson Teich amejiuzulu wadhfa wake, ikiwa si zaidi ya mwezi mmoja tangu akalie kiti hicho, kutokana na kile kilichoelezwa utata uliomo ndani ya serikali ya taifa hilo katika namna ya kulishughulikia janga la virusi vya corona. Waziri huyo anatajwa kuupinga mpango wa Bolsonaro wa kurefusha matumizi ya dawa ya malaria ya hydroxychloroquine kama tiba ya COVID-19, akionya itaweza kusababisha madhara zaidi.Mtangulizi wa Teich, Luiz Henrique Mandeta alijiuzulu kutokana na sababu kama hizo aliposhindwa kukubaliana na Rais Bolsnaro. Brazil yenye jumla ya watu milioni 200, ina maambukizi zaidi ya 200,000 na vifo 14,000 na kuifanya kuwa taifa la sita lenye vifo na maambukizi mengi duniani. Katika kipindi cha masaa 24 kumerekodiwa maambukizi mapya 15,300.

Mamia wanakufa Yemen kutokana na matatizo ya kupumua

Jemen Darwan Flüchtlingslager
Mkimbizi akiwa katika banda lake nchini YemenPicha: picture-alliance/AA/M. Hamoud

Nchini Yemen, zaidi ya watu 500 wamekufa katika kipindi cha siku nane zilizopita, wengi miongoni mwa hao vifo vyao vinatokana na matatizo ya kupumua. Hali hiyo iliyodhihirika katika mji wa Aden, inazusha wasiwasi wa kwamba taifa hilo lililovurugwa na vita vywa wenyewe kwa wenyewe, limeshindwa kabisa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. Mchimba kaburi mmoja aliliambia shirika la habari la AP, kwamba hajawahi kushuhudia idadi ya vifo kama hivyo katika kipindi chote cha miaka mitano ya vita nchini humo. Ujumbe wa pole umetolewa na watu mbalimbali katika mtandao wa Twitter na mingine ya kijamii, huku wengine wakionesha kufikwa na msiba zaidi ya mmoja kwa siku.

Huko Senegal baadhi ya misikiti imefungua milango yake hapo jana, baada ya serikali kuligeza masharti ya kukabiliana na kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona. Lakini baadhi ya misikiti hiyo inahisi bado kiwango cha maambukizi kipo juu na kusalia kufungwa. Wiki hii, Rais wa Senegal Macky Sall alisema ibada za umma zinaweza kuendelea katika taifa hilo, ingawa kwa misingi ya kanuni za kujitenga baina ya watu. Zaidi ya asilimia 90 ya raia wa taifa hilo ni Waislamu, wa madhehebu ya Sufi, ambao wanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika taifa hilo lenye jumla ya watu milioni 16. Nchini humo kumerekodiwa vifo 25 na maambukizi 2, 310.