1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinga mpya ya UKIMWI yafanyiwa majaribio Afrika Kusini

Zainab Aziz
1 Desemba 2016

Tarehe moja Disemba, dunia inaungana katika maadhimisho ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI. Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Mikono juu kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI".

https://p.dw.com/p/2TYaP
Welt-Aids-Tag 2016
Picha: picture alliance/dpa/P. Adhikary

Kila inapofika tarehe mosi mwezi Disemba kila mwaka dunia inaadhimisha siku y akimataifa ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.   Sindano ya kinga dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI inafanyiwa majaribio nchini Afrika Kusini ambako idadi ya watu wengi zaidi walio na maambukizi hayo inapatikana nchini humo.

Zaidi ya watu 1000 wanaambukizwa virusi vya HIV kila siku. Ugonjwa wa UKIMWI sio tena hukumu ya kifo kama ilivyoaminika hapo awali kwa sababu kuna dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo zinazojulikana kama ARV's  hata hivyo lakini wataalamu wanaamini kwamba maambukizi ya virusi vya HIV yanaweza kuangamizwa iwapo kutakuwepo na sindano ya kinga dhidi ya virusi hivyo.  Afrika Kusini imeshafanya majaribio kadhaa juu ya kinga hiyo na hapo jana nchi hiyo ilianzisha rasmi majaribio yenye matarajio makubwa. 

Mtaalamu akiwa ameshikilia kifaa cha chanjo ya UKIMWI mjini Pretoria
Mtaalamu akiwa ameshikilia kifaa cha chanjo ya UKIMWI mjini PretoriaPicha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Afrika Kusini

Hakuna nchi ambayo imeathiriwa zaidi na watu wanaoishi na virusi vya HIV kama Afrika Kusini.  Watafiti wengine wanazungumzia juu ya njia za kuhuzunisha.  Linda-Gail Bekker kutoka chuo kikuu cha Cape Town ndiye anayeongoza  utafiti huu mpya  anasema, ''kutafuta kinga ambayo itaweza kuzuia mtu kuambukizwa virusi vya HIV ni utafiti wa kina, tunajua kwamba hatuwezi kudhibiti au kuumaliza ugonjwa wa UKIMWI kabla ya kwanza kupata kinga ambayo itawakinga watu na maambukizi. Iwapo  mwishowe tutakuwa na uwezekano wa kupata kinga, utakuwa ni ushindi dhidi ya maradhi hayo.''

Zoezi hilo la majaribio ya kinga ni zoezi lenye nguvu ambalo limehusisha maeneo 15 ikiwa ni pamoja na Cape Town, Durban na Pretoria. Majaribio hayo yako katika sehemu yake ya tatu na kiwango kikubwa cha watu wapatao 5,400 wameshafanyiwa majaribio hayo.  Wote ni watu walio na umri kati ya miaka 18 na 35.  Theluthi mbili kati yao ni wanawake kwa sababu wao ndio wanaoathirika zaidi. Linda Gail amesema kuwa ni jambo jema kwa Afrika Kusini kuwa ndio nchi iliyochaguliwa kufanyika majaribio hayo.

''Kwanini hapa? hii ni kama mseto wa matambu na machungu kwa sababu Afrika Kusini ina mzigo mzito wa HIV'', amesema mtafiti huyo na kuongeza kuwa ''hii si habari nzuri lakini jambo zuri ni kwamba utafiti unafanyika hapa, miundo mbinu tunayo, watalaamu tunao na washiriki ambao wanataka kuona UKIMWI umeangamizwa wapo.''

Chanjo ya HVTN 702 

Vifaa vya kupima UKIMWI kama vinavyoonekana katika mashine za manunuzi
Vifaa vya kupima UKIMWI kama vinavyoonekana katika mashine za manunuziPicha: Reuters/Str.

Chanjo hiyo ni msingi wa utafiti ambao ulifanywa miaka saba iliyopita nchini Thailand, hiyo inamaanisha kuwa wakati huo njia zilizotumika zilikuwa zimeboreshwa na wakati huu matumaini yenye mafanikio yanatarajiwa.  Anthony Fauci mtaalamu wa Kinga ya mwili kutoka Marekani anazungumzia juu ya utafiti muhimu ambao yeye ana matumaini makubwa.

Fauci amesema, ''tutafaulu kinachotokea hivi sasa katika utafiti wa Afrika Kusini ni muendelezo wa awali wa kinga ya RV 144. Labda hatutaweza kufikia lengo kuu lakini naamini na nina matumaini changamoto tutazishinda hiyo inaonekana wazi", anamalizia mtaalamu huyo kutoka Marekani.

Aidha, Anthony Fauci ameendelea kuelezea kuwa kinga salama na ya uhakika itakuwa sawa na msumari wa mwisho kwenye jeneza la HIV. Kwa mara ya kwanza watafiti wengine wanasema kuwa inaonekana kuna uwezekano.

Linda Gail Bekker pia ana matumaini makubwa ya kupata ushindi, na hilo litakuwa ni jambo la muhimu anasema kwa sababu vijana nchini Afrika Kusini hawapendi kuzungumzia UKIMWI tena.  Hata hivyo utafiti unahitaji muda na matokeo hayatapatikana mpaka mwisoni mwa mwaka 2020.

Mwandishi: Jana Genth/Zainab Aziz.

Mhariri: Daniel Gakuba