1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga chasababisha vitu na madhara Bangladesh

Maja Dreyer16 Novemba 2007

Tangu kimbunga cha Sidr kilipoanza kushambulia eneo la pwani ya Kusini mwa Bangladesh, idadi ya watu waliouawa katika janga hilo inazidi kuongezeka. Hata hivyo, idadi ya wale waliookolewa ni kubwa zaidi.

https://p.dw.com/p/CImi
Watu wanachunguza nini kilichobaki baada ya kimbunga kushambulia makaazi yao
Watu wanachunguza nini kilichobaki baada ya kimbunga kushambulia makaazi yaoPicha: AP

Pamoja na upepo mkali wa kasi ya zaidi ya kilomita 200 kwa saa, eneo la Kusini mwa Bangladesh lilikumbwa pia na mafuriko. Maji yalikuwa mita tano kuliko kima cha kawaida. Afisa husika wa wizara ya msaada na usimamizi wa maafa alisema idadi ya watu waliouawa inaweza kuwa kubwa sana kuliko invyojulikana hivi sasa.

Wasaidizi bado hawakuweza kufika katika maeneo mengi yaliyoathirika zaidi na kimbunga hiki cha “Sidr” kwa sababu ya mafuriko pamoja na miti na waya za umeme zinazoanguka zinazuia barabara kutumika. Huduma za umeme na simu ziliharibika, kwa hivyo maafisa wa kusimamia hali ya dharura wanatumia simu za mkono kuzungumza na maafisa wa mikoa na kupata habari zaidi juu ya hasara na idadi ya watu waliouawa.

Ingo Ritz, ambaye ni mfanyakazi wa shirika moja la Kijerumani lisilo la kiserikali ambalo linajihusisha Bangladesh, yuko katika eneo la Dhaka, Bangladesha hivi sasa Naye anaeleza hivi juu ya matokeo ya kimbunga hiki ambacho kimetokea miezi michache tu baada ya mafuriko makubwa yaliyowaua watu 1000: “Madhara makubwa yaliyotokea safari hii, pamoja na waliouawa, ni kuharibika kwa nyumba nyingi. Hivi punde tu nimezungumza na Bibi mmoja anayetoka kijiji kidogo nje ya Dhaka ambapo mabanda mengi yalivunjwa, mapaa yaliruka. Hali ni mbaya zaidi kwenye eneo la pwani ambapo yalitokea pia mafuriko. Tatizo jingine ni kuharibika kwa mavuno. Wakati huu, mpunga umekomaa, na haukuvunwa. Kwa hivyo, kutakuwa na uhaba wa vyakula na bei ya mchele itapanda nchini kote.”

Wataalum walikadiria kuwa kimbunga hiki “Sidr” kilikuwa na nguvu sawa na kimbunga kilichotokea mnamo mwaka 1991 ambapo takriban watu 140,000 waliuawa. Kabla ya hapo, kimbunga kingine kiliwaua watu laki tano hapo mwaka 1970 nchini Bangladesh.

Tokea wakati huo nchi hii imeanzisha kituo cha kutabiri uwezekan wa kutokea kimbunga kwa madhumuni ya kuwaonya wakaazi pamoja na kujenga nyumba za kimbilio katika eneo la pwani. Watu millioni moja hivi walihamishwa kutoka nyumba na mabanda yao katika vijiji vya pwani kabla ya kimbunga hiki cha jana. Juu ya hayo, viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mashua za kuvushia vilifungwa. Wasaidizi walitumia vipaza sauti ili kuwa onya wavuvi juu ya hatari inayotajariwa. Kutokana na mbinu hii inasemekana kwamba mamia ya maisha ya watu yalihifadhiwa.

Nchini India pia, watu laki moja hivi walihamishwa kutoka eneo la pwani. Kimbunga “Sidr” kilipunguza uzito wake na kutosababisha hasara nyingi huko India. Waziri wa msaada wa mkoa wa West Bengal ulioko mpakani na Bangladesha alisema zaidi ya mabanda 100 ya udongo yalivunjika na mvua ilisababisha madhara fulani katika misitu ya mikoko.