1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kilio cha vijana wa dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Oumilkheir Hamidou
20 Septemba 2019

Viongozi wa dunia wakijiandaa kwa mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi mjini New-York, mamilioni ya vijana wa dunia hawajenda shule au kazini wanaandamana kudai hatua za dharura dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

https://p.dw.com/p/3Pvh3
BG FFF weltweit | Kenia| Klimastreik | Global Strike 4 Climate | Nairobi
Picha: Reuters/B. Ratner

Maandamano yaliyoanzishwa na msichana wa miaka 16 wa Sweeden, mwanaharakati Greta Thunberg yanafanyika katika nchi zisizopungua 150 . Lengo la wanafunzi na vijana wengine wa kutoka kila pembe ya dunia ni kuzungumza kwa sauti moja kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kuiathiri sayari yetu.

"Jua lilipochomoza, Septemba 20 mwaka 2019  vijana wa Australia, walikuwa wa mwanzo kuteremka majiani wakifuatiwa na wenzao wa Ufilipino, Japan na visiwa vya bahari ya Pacific. Katika risala yake kupitia mtandao wa Instagram Greta Thunberg amewatakia kila la kheri .Binafsi mwanaharakati huyo ataongoza maandamano kama hayo mjini New-York yanakokutikana makao makuu ya Umoja wa mataifa. Wanafunzi zaidi ya milioni moja na laki moja wanatarajiwa kuhudhuria maandamano hao. Mjini Bonn pia nchini Ujerumani vijana na watu wazima, wakiwemo waandishi habari na watumishi jumla wa DW wameandamana hadi katika jengo la Umoja wa mataifa inakokutikana ofisi kuu inayoshughulikia masuala ya mazingira.

 

Bibi mmoja anapita mbele ya bunge la Ujerumani, akibeba bango lenye maandishi" amueni sasa"
Bibi mmoja anapita mbele ya bunge la Ujerumani, akibeba bango lenye maandishi" amueni sasa"Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Serikali kuu ya Ujerumani yakubaliana kuhusu hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Waandalizi wanasema maandamano yana sura tofauti lakini lengo ni moja nalo ni kuwaziduwa walimwengu juu ya hatari ya mabadiliko ya tabianchi na kuhimiza hatua madhubuti zichukuliwe kuzuwia madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kwa maneno megine kupunguza moshi unaotoka viwandani.

Nchini Ujerumani ambako maandamano kama hayo yanafanyika katika miji tofauti , baraza la mawaziri lilijadiliana hadi usiku kucha kuhusu mipango ya kuinusuru sayari yetu. Duru za kuaminika zimeliambia shirika la habari la dpa kwamba baada ya masaa 15 ya majadiliano uwezekano ni mkubwa sasa wa kufikia makubaliano kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na kupandisha bei ya mafuta na kupanua vyanzo vya nishati mbadala.

Kwa mujibu wa wanasayansi kuzidi hali ya ujoto inayosababishwa na moshi wa sumu unaotoka viwandani ndio chanzo cha joto kali na ukame, thelevu kuyayuka ,vipimo vya maji ya bahari kupanda na kusababisha mafuriko.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa

Mhariri: Iddi Ssesanga