1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kilimo chaanza kunufaisha baadhi ya Mataifa Afrika

8 Septemba 2016

Ripoti ya muungano wa mabadiliko ya kijani Barani Afrika AGRA inaonesha kuwa nchi za kiafrika zilizochukua hatua mapema kuwekeza katika kilimo zimeanza kunufaika kutokana na kuongezeka kwa uchumi na kupunguza utapiamlo

https://p.dw.com/p/1Jxp7
Burundi Landwirtschaft
Baadhi ya wakulima nchini BurundiPicha: picture-alliance/Ton Koene

Ripoti hiyo iliyotolewa siku ya jumanne jijini Nairobi nchini Kenya imesema kuwa kwa miongo kadhaa nchi nyingi za kiafrika ambazo zilikuwa zimekumbwa na kudumaa kwa uchumi sasa zimeanza kufurahia kilimo endelevu ambacho kimeongeza uzalishaji na hivyo kuchangia kuongezeka kwa pato la ndani GDP kwa asilimia 4.3 wakati zile ambazo hazikuchukua hatua hiyo zikitajwa kukua kwa kwa asilimia 2.2 tu

Mafanikio hayo katika kilimo yanatajwa kuwa ni njia muhimu katika kupunguza umasikini ikilinganishwa na mafanikio katika sekta nyingine katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara kwa sababu kilimo ni njia kuu ya kujiongezea kipato kwa zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi na pia kilimo kinabaki kuwa njia pekee ya ajira kwa watu katika mataifa mengi Afrika kwa miongo kadhaa sasa

Kwa upande mwingine ripoti hiyo inasema utapiamlo umepungua katika nchi hizo kwa wastani wa asilimia 3.1 wakati nchi ambazo hazikuwekeza katika mbinu hizo utapiamlo umetajwa kupungua kwa asilimia 1.2 pekee

Landwirtschaft in Afrika
Mkulima nchini Tanzania akitengeneza njia ya maji katika shamba lakePicha: AP

Kilimo katika nchi za kiafrika kinakabiliwa na changamoto kubwa ya uzalishaji mdogo kutokana na kukosekana kwa mbegu sahihi na mbolea ambazo zitawawezesha wakulima kupata mazao mengi zaidi lakini pia kupungua kwa maji kutokana kutokuwepo kwa mvua za kutosha, pamoja na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali kama vile ukame ambao huathiri mazao na uzalishaji wa samaki

David Ameyaw kiongozi wa timu ya ufuatiliaji na tathimini kutoka katika muungano wa mabadiliko ya kijani akiwa pia ni mmoja kati ya walioandika ripoti hiyo,amesema kuwa kuna haja ya kuongeza kuhudi zaidi mpaka itakapofika 2030 ili kuwe na mabadiliko yenye maana kubwa katika sekta ya kilimo na kuongeza kuwa nchi hizo zimefanikiwa licha ya kuwa Serikali za hazikutenga bajeti ya asilimia 10 kama walivyokuwa wamekubaliana kwa ajili ya kuboresha kilimo katika nchi zao

Na hivyo kuna haja ya wakulima kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji zaidi pamoja na kuwa tafiti zinaonyesha kuwa kuna asilimia 1 mpaka 3 ya wakulima wanaojihisisha na kilimo cha umwagiliaji katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara

Ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2014 ilionyesha kwa theluthi mbili ya wakulima wadogo katika nchi za Ethiopia,Malawi,Niger, Nigeria, Tanzania na Uganda hawakutumia mbolea zenye kemikali katika kilimo

Uwekezaji zaidi katika kilimo unahitajika

Nchi 13 pekee za kiafrika zilifikia lengo hilo na ikiwa kutakuwa na uwekezaji wa kutosha katika nchi zilizosalia uwekezaji katika sekta ya kilimo utaongezeka na kufikia dola bilion 12 za kimarekani

Huku ikizitaja nchi zilianza kutumia program hiyo mapema kati ya mwaka 2007 na 2009 ni Benin Burundi, Cape Verde, Ethiopia na Gambia, nchi nyingine ni Ghana, Liberia, Mali, Niger, Nigeria Rwanda Sierra Lione na Togo

Inaelezwa kuwa uwekezaji katika kilimo unahitaji utashi wa kisiasa, uwepo wa sera na teknolojia ambayo itasaidia kukibadilisha kilimo ili kiwe na tija, upatikanaji wa mikopo kwa wakulima pamoja na uhakika wa soko kwa ajili ya bishaa zao.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu