Kenyatta, Ali na Muthaura kurudi ICC Septemba 21
8 Aprili 2011Washukiwa hao Uhuru Kenyatta, Francis Muthaura na Hussein Ali walifika mahakamani mwendo wa saa nane na nusu alasiri. Watatu hao wanadaiwa kuwa waliipanga njama iliyosababisha ghasia baada ya uchaguzi mkuu katika maeneo ya Naivasha na Nakuru. Jaji anayeongoza mchakato dhidi ya watuhumiwa wa ghasia hizo Ekaterina Trendafilova, aliwaonya washukiwa hao wasitoe kauli za uchochezi zitakazoleta vurugu kwani kauli hizo zinaweza kuifanya mahakama ya ICC kutoa waranti wa kukamatwa kwao.
Jaji Trendafilova, Alhamisi aliwasomea madai dhidi yao mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto aliyekuwa waziri wa viwanda, Henry Kosgei na mtangazaji wa kituo cha redio cha Kass Fm Joshua arap Sang. Baadaye mahakama hiyo ilitangaza kwamba watatu hao wataijua hatma yao Septemba mosi ikiwa watasimama kizimbani kujibu kesi dhidi yao au la.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya
Mhariri: Josephat Charo