1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na juhudi za upatanishi

7 Februari 2008

Juhudi za upatanishi nchini kenya zapamba moto huku mawaziri wa nje wa nchi jirani wakiwasili Nairobi kuhimiza suluhisho.

https://p.dw.com/p/D3o4

Wapinzani wa kisiasa wa pande mbili zinazohusika na mgogoro wa kenya wameendelea na mazungumzo yanayoungwamkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kukomesha wiki kadhaa za machafuko ya umwagaji damu.Kwa upande mwengine, mawaziri wa nje wa nchi za Afrika mashariki wamewasili nao leo mjini Nairobi kutilia nguvu juhudi za amani. Marekani imewapiga marufuku wanasiasa 10 wa Kenya kuingia Marekani huku ujumbe wa Umoja wa mataifa umewasili leo kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu humo nchini.

Katika mazungumzo ya jana yaliongozwa na Katibu mkuu wa zamani wa UM Kofi Annan,wajumbe wanaomuakilisha rais Kibaki na wale wa upinzani wanaomuakilisha Raila Odinga walizungumzia maswali ya kimsingi yanayohusiana na matokeo ya uchaguzi wa rais wa desemba mwaka jana.

Baraza la Usalama la Um limeungamkono kwa nguvu jitihada za amani zinazoongozwa na Katibu mkuu wa zamani wa UM Kofi Annan ili kukomesha machafuko ya kikabila yalioikumba Kenya na likawataka viongozi wanaopingana nchini kuhimiza suluhu nchini.

Baraza la Usalama la UM lenye wanachama 15 kwa sauti moja limepitisha taarifa ikielezea wasi wasi mkubwa kwamba licha ya

Ahadi walizotoa hapo Februari mosi,raia wanaendelea kuuwawa ,wanawake wanabakwa na wakaazi wanaendelea kutimuliwa kutoka maskani zao.

Mawaziri wa nje wa nchi jirani za Afrika mashariki-Uganda,Djibouti,Somalia,Ethiopia na Sudan wamewasili kwa mkutano wa leo ambao afisa wa wizara ya nje ya Kenya ameutoa hadhikuwa ni kama ni jukwaa la kushauriana tu.hii inafuatia malalmiko kutoka upinzani.

Upinzani ulidai mkutano unaoandaliwa na serikali ni njama ya Kibaki kuataka kutambuliwa kama rais .Upinzani ukatishia kufanya maandamano majiani.

Jana upinzani ulivunja maandamano hayo baada ya serikali kuridhia na kusema kuwa mawaziri hao wa nje wa nchi hizo hawatakutana rasmi na serikali kama sehemu ya kikundi cha IGAD.

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika mashariki unapangwa kufanyika kesho ijumaa kwa lengo la kutathmini maendeleo yaliofikiwa katika upatanishi wa Annan na kujaribu kizihimiza pande zote mbili kuendelea kujitolea kidhati kwa mazungumzo.Msemaji wa wizara ya nje ya Kenya alisema mipango ya mkutano huo wa kilele utakaohudhuriwa na viongozi wa Uganda,Tanzania,Burundi na Rwanda inabidi bado kukamilishwa.

Nae kamishna wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya Louis Michel ameelekea pia nairobi akisema anaamini maendeleo makubwa ya kisiasa katika mazungumzo haya yatapatikana mnamo siku chache zijazo na kwamba UU uko tayari kuungamkono suluhisho la kisiasa litakaloibuka.

Kofi Annan alitoa muda wa siku 15 kuutatua mgogoro wa Kenya uliozuka kutokana na uchaguzi wa desemba 27 ambao Upinzani umedai ulifanyiwa mizengwe.

Magharibi ya Kenya imebakia katika hali ya machafuko huku polisi ikiripoti kuuwawa kwa watu 19 katika mapigano yaliozuka tangu jumapili huko Rift alley.Watu 12 wameuwawa katika eneo hilo hilo juzi jumaane.

Tume ya kutafuta ukweli ya UM imewasili nayo kenya kutathmini tuhuma za kukanyagwa haki za binadamu tangu uchaguzi wa urais.Isitoshe,Marekani imetangaza leo inawanyima viza za kutembelea Marekani wanasiasa 10 mashuhuri tangu wa serikali hata wa upinzani kwavile wamehusika na kuchochea ghasia tangu uchaguzi wa Desemba 27 mwaka jana.