1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karzai ataka kukutana na Mullar Omar

A.Liongo30 Septemba 2007

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa makundi ya Taliban na Hezb Islam katika juhudi za kutafuta amani nchini humo.

https://p.dw.com/p/CH7S

Rais huyo pia ametoa changamoto kwa viongozi hao Mullar Mohamed Omar wa Taliban na Gulbuddin Hekmatyar wa Hezbi Islam kushiriki katika uchaguzi mkuu ujayo.

Amesema kuwa ikiwezakana atawapa nafasi ya uongozi katika baraza lake la mawaziri kama watahitaji.

Hata hivyo wapiganaji hao wa kitaliban wamekuwa wakidai kuwa kabla ya mazungumzo kufanyika ni lazima majeshi ya kigeni yaondoke kwanza, kitu ambacho Rais Karzai amesisitiza kuwa hatokikubali.

Kauli hiyo ya Rais Karzai imekuja muda mfupi baada ya kutokea shambulizi kubwa la bomu la kujitoa mhanga ambapo kiasi cha watu 30 wengi wakiwa ni askari wa jeshi la Afghnaistan kuawa mjini Kabul.

Kundi la Taliban limedai kuhusika na shambulizi hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa toka mwaka 2001 ambapo Rais Karzai alisema kuwa angetamani kuwauliza viongozi wa Taliban kwanini wanajaribu kuisambaratisha nchi.

Msemaji wa wizara ya Ulinzi ya Afghanistan General Zahir Azimi amesema kuwa askari wengine 21 walijeruhiwa katika shambulizi hilo, ambapo mshambuliaji aliyeva sare za jeshi alijilipua baada ya kuingia ndani ya basi hilo.

Zaidi ya watu elfu 3 wameuawa nchini Afghanistan mwaka huu ambapo majeshi ya nchi hiyo yakisaidiwa na yale ya NATO yamekuwa yakipambana na wapiganaji wa Kitaliban.