1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yafikia muafaka kuhusu tabia-nchi

Mohammed Khelef/ZPR11 Desemba 2011

Mataifa 194 yanayowakilishwa kwenye mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu tabia-nchi mjini Durban yamefikia makubaliano yatakayozifanya nchi zote kupunguza hewa chafu chini ya mkataba mpya kufikia mwaka 2017.

https://p.dw.com/p/13QiQ
Alama ya mti wa mbuyu iliyotumika katika mazungumzo ya tabia-nchi.
Alama ya mti wa mbuyu iliyotumika katika mazungumzo ya tabia-nchi.Picha: picture-alliance/dpa

Mkataba wa Kyoto wa mwaka 1997 ambao unafikia kikomo chake mwakani lakini hauwashirikishi wachafuzi wakubwa wa mazingira duniani - Marekani, China na India - unaonekana kuongezewa muda katika kipindi hicho cha mpito.

Vyombo maalum vitawekwa kukusanya na kugawanya mabilioni ya euro kwa mataifa masikini ili kuyasaidia kukabiliana na kuongezeka kwa joto ulimwenguni. Mkutano huo wa Durban ulilazimika kurefushwa kwa siku mbili huku mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane, akitangaza kwamba kumefikiwa muafaka.

Rasimu ya muafaka huo ambao umetokana na makubaliano ya Umoja wa Ulaya na kuungwa mkono na mataifa mengi inataka hadi kufikia mwaka 2020, pawepo na nguvu za kisheria kusimamia makubaliano ya kimataifa kuhusiana na tabia-nchi.

Makundi ya utetezi wa mazingira duniani, yakiwemo ya Greenpeace na WWF, yamesema kwamba kilichopatikana kutoka Durban ni makubaliano ya hiari tu ambayo yanachelewesha hatua za pamoja kuzuia janga la kuongezeka kwa joto ulimwenguni. Kamishna wa Umoja wa Ulaya, Connie Hedegaard, amesema pande zote zililazimika kuwa tayari kwa hatua za kisheria.