1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani nchini Somalia

Oummilkheir6 Machi 2007

Kundi la mwanzo la wanajeshi wa Umoja wa Afrika wawasili MOgaadischu

https://p.dw.com/p/CHIt
Polisi wa kisomali mjini Mogadischu
Polisi wa kisomali mjini MogadischuPicha: AP

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika wamewasili kwa mara ya kwanza katika mji mkuu wa Somalia-Mogadischu alfajiri ya leo.

Ndege mbili chapa ANTONOV zilizokua na wanajeshi wa Uganda na vifaa vya kijeshi,ikiwa ni pamoja na vifaru,zimetuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Mogadischu ambako hatua za ulinzi zimeimarishwa.

Wanajeshi kama 16 hivi wa Uganda walilahikiwa na mkuu wa jeshi la Somalia,jenerali Abdullahi Omar Ali,waziri wa mambo ya ndani Muhamud Ahmed Guled,naibu waziri wa ulinzi Salad Ali Jelle na maafisa wa jeshi la Ethiopia,ambao nchi yao inaisaidia serikali ya Somalia kujaribu kuleta amani nchini.

Kundi la mwanzo la walinzi wa amani wa Umoja wa Afrika-maafisa kama 30 hivi wa kutoka Uganda,waliwasili March mosi iliyopita mjini Baidoa,umbali wa kilomita 250 kaskazini magharibi ya mji mkuu Mogadishu-kunakokutikana pia bunge la Somalia.

“Kuwasili wanajeshi wa Umoja wa Afrika kunaniliwaza.Watasaidia bila ya shaka kuleta hali ya utulivu na kuwapatia mafunzo wanajeshi wetu ili tuweze kujihami wenyewe” amesema jenerali Abdullahi Omar Ali aliyewasifu wanajeshi wa umoja wa Afrika kua ni fursa ya aina pekee kwa wananchi wa Somalia na kwa eneo jumla la pembe ya Afrika.

Akitangaza habari za kutumwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia,kamishna wa Umoja huo anaeshughulikia masuala ya amani na usalama ,Said Djinnit,amesema lengo la wanajeshi hao ni kuwasaidia wasomalias Bwana Said Djinnit amesema:

“Tume ya amani ya Umoja wa Afrika imeshakwenda Mogadschu leo asubuhi .”Tume ya Umoja wa Afrika iko huko ili kuwasaidia wasomali wote.Hakuna njia nyengine ya kufikia amani na utulivu nchini Somalia,isipokua juhudi za kisiasa na majadiliano.

“Serikali kuu ya mpito inahitaji msaada mkubwa kuweza kulifikia lengo hilo”amemaliza kisema kamishna wa Umoja wa Afrika anaeshughulikia masuala ya amani na usalama Said Djonnit.

Wanajeshi hao wa Uganda ni sehemu ya mwanzo tuu ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika.Nigeria,Ghana,Malawi na Burundi zimeelezea pia utayarifu wa kushiriki katika juhudi za kulinda amani nchini Somalia.

Jeshi hilo la Umoja wa Afrika litakalokua na wanajeshi kama elfu nane litashika nafasi ya vikosi vya Ethiopia vilivyowasaidia wanajeshi wa serikali ya Somalia mwezi December mwaka jana,kuwatimua wanamgambo wa mahakama za kiislam waliokua wakiudhibiti mji mkuu Mogadischu na sehemu kubwa ya kusini mwa Somalia.

Hali ni tete nchini Somalia na Mogadishu umegeuka uwanja wa hujuma za kila kukicha dhidi ya vikosi vya serikali na washirika wao wa Ethiopia.

Wanamgambo wa itikadi kali wameshaonya watawashambulia pia wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa Afrika.