1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joachim Löw kabla ya kutawaza

Sudi Mnette
30 Mei 2018

Kocha Joachim Löw  ni mtu  mwenye  kuangalia mbali, Mtu wa mawasiliano, Mfanyakazi wa mahusiano na Umma. Hivyo ndivyo  Joachim Löw  alivyo katika jukumu lake muhimu kama Kocha wa taifa

https://p.dw.com/p/2yeOJ
Eppan DFB WM Trainingslager Südtirol Jogi Löw
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Anapaswa kulielewa. Amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka kumi na mbili sasa, takriban sawa na alivyo Angela Merkel kama Kansela wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Jogi kama anavyoitwa kwa mkato akiwa na fulana yake iliokatwa  alama ya V shingoni na anayezungumza Kijerumani kwa lafdhi ya Kusini mwa Ujerumani , ameshika wadhifa wa kocha wa timu ya taifa ya Kandanda, kwa kisiasi ambacho Mjerumani  hakumbuki mtu mwengine-hakuna mashindano ya kandanda bila ya yeye kuwepo. Hivi sasa amerefusha mkataba wake na Chama cha kandanda cha Ujerumani (DFB) safari hii hadi 2022, yatakapofanyika mashindano  mengine ya Kombe la dunia baada ya 2018.

Kwanini anafanya hivyo  wakati yeye ni bingwa mtetezi aliyekwisha tunzwa medali ya juu ya Ujerumani ya utumishi uliotukuka  na mtu aliyekwisha chaguliwa Kocha wa mwaka wa Shirikisho la Kandanda la Kimataifa –FIFA na hata uwanja wa michezo wa kwao anakotoka kupewa jina lake ? wakati hayo yakimpa motisha kusonga mbele, kwa hakika hana cha kupoteza.

Kubwa muhimu  Katika Timu:

Trainingslager Deutsche Nationalmannschaft
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw Picha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

"Kombe la  Dunia 2014 yalikuwa mafanikio ya juu kabisa kwetu sote lakini sio mwisho,” anasema  Löw mwenye umri wa miaka 58. Ushindi mmoja hautoshi anataka kukamilisha kile  ambacho hakijawahi kutimizwa na  kocha mwengine wa timu ya taifa kabla yake na ambacho hadi sasa ni mataifa mawili tu yameweza kukifanya  Itali(1938) na Brazil (1962) . Kuutetea ubingwa wa kombe la dunia na kulinyakua tena. Katika mahojiano na DW, Löw amesema " Kuendelea  kuwa  katika kiwango hicho cha juu, kunahitaji jitihada kubwa”.

Bila shaka  unaposherehekea mafanikio mengi, ni dhahir  unafika mahali shauku inapotea ni jambo la kibinaadamu. Kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha unafikia kiwango cha juu bila ya kuporomoka. Löw ana imani na timu yake ambayo pia imekuwa  na ujuzi mkubwa, jambo ambalo lilikuwa nadra kwa timu ya Ujerumani hapo kabla. " Bado naona uwezo mkubwa ndani ya timu hii na bado nina hamu kubwa ya kuendelea kufanya kazi na kikosi hiki cha wachezaji, nikiwaendeleza zaidi”.

Mbali na hayo, Löw anajuwa kujivunia  kuwa kocha wa timu ya taifa asiyepingika na hujiepusha na  shinikizo, jambo ambalo huwakumba makocha wengine wanapofanya juhudi za kutafuta mafanikio. Anaweza kufanya kazi kwa utulivu kabla ya  Kombe la Ulaya na Kombe la dunia na bila ya shinikizo kutoka juu. Hayo humsaidia kufikiria jinsi ya kujipanga kwa muda wa wastani au muda mrefu kwa mikakati yake mwenyewe,fikra,falsafa ya mchezo na mbinu za mchezo, pamoja na  maendeleo mapya ya kandanda na uchambuzi .

Shauku ya ushindi

Löw anasema ,” huenda tukawa na kitu  ambacho wengine watakiona cha kiwenda wazimu katika kombe la dunia nchini Urusi, lakini ni katika kutafuta  mbinu mpya na  ndiyo maana tunazingatia sana mustakbali wetu ". Anasema  hata mashabiki wa Ujerumani huwa na shauku kwa sababu  kiwango katika mechi nne zilizopita , dhidi ya  England, Ufaransa, Uhispania na Brazil hakikuwa cha kuvutia. Hao wote ni washiriki wakubwa katika Kombe la dunia. Tulitoka sare mara tatu na  kupoteza mechi moja, lakini hupaswi kuanza kuwa na wasiwasi anasisitiza kocha Löw.

Löw amekuwa akijiandaa  vilivyo kwa matayarisho ya  Kombe la Dunia tangu kiasi miaka miwili iliopita. Mwenyewe anasema bila ya mipango hakuna mafanikio, lakini ukiwa na akili iliotulia unaweza kupiga hatua kubwa  mbele. Anamaliza kwa kusema,  pamoja na yote mashabiki wa kandanda wa Ujerumani wanapaswa kuwa  na matumaini na wakati huo huo na tahadhari kwani kuna  wakati ambapo mafanikio huwa ni suala la bahati.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/Wiertz,Sarah ( DW Sport)

Mhariri: Grace Patricia Kabogo