1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joachim Gauck hatogombea tena urais

Hamidou Oummilkheir6 Juni 2016

Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, hatowania muhula wa pili, akianzisha kinyang'anyiro cha nani atakaemrithi na wakati huo huo kuvuruga hesabu za uchaguzi, miezi 15 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

https://p.dw.com/p/1J1Qd
Rais wa shirikisho Joachim Gauck akizungumza na waandishi habari katika kasri la Schloß Bellevue
Picha: Reuters/H. Hanschke

Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck amesema umri wake ndio chanzo cha kuamua asigombee mhula wa pili mwezi februari mwaka 2017. Akizungumza na waandishi habari katika kasri lake la Bellevue mjini Berlin rais Joachim Gauck ambae hivi sasa ana umri wa miaka 76 amesema:"Leo nnapendelea kukuarifuni kwamba nimeamua,nisipiganie tena mhula mwengine wa rais wa shirikisho. Uamuzi huo haukuwa rahisi kwangu,kwasababu ni heshima kubwa kwangu kupata fursa ya kuitumikia nchi hii,nchi yetu,shirikisho la jamhuri ya Ujerumani."

Hata kama wadhifa wake kwa sehemu kubwa ni wa heshima,kuanzia uongozi wa kimaadili na kuiwakilisha Ujerumani nchi za ng'ambo,Gauck,aliyechaguliwa mwaka 2012 kwa mhula wa miaka mitano,hakuchelea kuchukua msimamo katika jukwaa la ndani la kisiasa,naiwe kwa kuunga mkono sera za kuwapokea wakimbizi au kwa kuzungumzia majukumu ya kihistoria ya nchi hii.

Kinyang'anyiro cha nani awe rais wa shirikisho kinaanza

Kwa kutangaza rasmi uamuzi wake ambao vyombo vya habari vimekuwa tangu siku kadhaa sasa vikiashiria,analifungulia njia "Baraza la shirikisho"pale wabunge wa shirikisho na wawakilishi wa mabaraza ya majimbo watakapokutana kumchagua mtu atakaeshika nafasi yake mwezi Februari mwakani.

Joachim Gauck akiondoka baada ya kutoa taarifa yake
Joachim Gauck akiondoka baada ya kutoa taarifa yakePicha: Reuters/H. Hanschke

Kwasasa hakuna chama chochote chenye wingi mkubwa kuweza kumchagua mgombea wake,inamaanisha pengine duru tatu za uchaguzi zitahitajika hadi rais mpya atakapochaguliwa. Zoezi hilo la uchaguzi linaashiria pia malumbano makali katika wakati ambapo kila chama tayari kimeanza kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa msimu wa mapukutiko mwakani na ambao kansela Angela Merkel bado hajatangaza dhamiri yake.

Kansela Angela Merkel atakaekutana baadae hii leo na rais wa shirikisho Joachim Gauck,anaweza kuchagua mgombea ama kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU au kumtafuta mtu mwenye nafasi nzuri ya kuungwa mkono na vyama vyingi vya kisiasa. Majina kadhaa yamekuwa yakitajwa na vyombo vya habari ikiwa ni pamaoja na spika wa bunge la shirikisho, Bundestag, Norbert Lammert wa chama cha CDU na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble.

Mwanamke wa kwanza kuwa rais wa shirikisho

Kansela Merkel anaweza pia kumgeukia Gerda Hasselfeldt wa chama cha CSU na kwa namna hiyo kuwa sababu ya kutuliza mvutano wa miezi kadhaa pamoja na chama hicho cha kusini mwa Ujerumani. Jina jengine la mwanamke linalotajwa ni lile la waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen,lakini wadadisi wanaamini lengo lake ni kuweza siku moja kumrithi kansela Angela Merkel.

Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen anapewa nafasi nzuri ya kumrithi rais Joachim Gauck
Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen anapewa nafasi nzuri ya kumrithi rais Joachim GauckPicha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Wadhifa wa rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ni wa heshima. Anaweza kuchaguliwa tena mara moja tu. Raia yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka 40 anaweza kugombea wadhifa huo.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga