1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lapambana na waandamanaji Syria

Halima Nyanza(ZPR)19 Agosti 2011

Majeshi ya Syria jana yalifyatua risasi kuwatawanya waandamanaji wanaoipinga serikali katika mji wa Homs ulioko katikati ya nchi hiyo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mwingine kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/12JLh
Wanajeshi wa Syria mitaaniPicha: picture alliance / dpa

Ghasia hizo zimetokea wakati ambapo, mapema jana rais wa Syria Bashar la Assad, alimwambia Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kwamba majeshi yake yamemaliza operesheni yake dhidi ya vuguvugu hilo linalotaka mabadiliko.

Unruhen in Syrien
Waandamanaji nchini SyriaPicha: picture alliance/dpa

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo wamefahamisha kuwa majeshi ya ulinzi pia yalisambazwa katika maeneo tofauti, ikiwemo katika vitongoji vya mji mkuu wa nchi hiyo Damascus, ambako kuliripotiwa maandamano na milio ya risasi kusikika.

Marekani na Umoja wa Ulaya tayari zimetoa kauli ya kumtaka rais Assad ajiuzulu. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema mashambulio makali yanayofanywa na jeshi la rais Assad, dhidi ya upinzani, ni kuonesha wazi kwamba utawala wake umekosa uhalali.

Syrien Präsident Bashar Assad 24.04.2011
Rais wa Syria Bashar AssadPicha: picture-alliance/dpa

Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Ureno zilisema jana kuwa zitalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Syria kutokana na mashambulio yanayosababisha vifo vya raia.

Umoja wa Mataifa umepanga kutuma ujumbe wake nchini Syria mwishoni mwa juma hili kutathmini hali ya kibinadamu.