1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Rais Abbas amekutana na waziri mkuu Ehud Olmert

28 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBV4

Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, amekutana leo na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, mjini Jerusalem.

Rais Abbas amemuonya Olmert kwamba mkutano wa mashariki ya Kati uliopendekezwa na Marekani kuhusu kuufufua mchakato wa kusaka amani huenda usiwe na maana yoyote.

Abbas amesema mkutano wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, hautakuwa na maana kama utazingatia tu kutangaza kanuni.

Ehud Olmert alimualika rais Abbas kwenye ikulu yake mjini Jerusalem kwa mazungumzo yaliyohusu kuziendeleza taasisi za Palestina, kuisaidia serikali ya rais Abbas na maswala ya Waisraeli na Wapalestina wanaoishi pamoja.

Rais Abbas na Ehud Olmert walikutana mara ya mwisho mnamo tarehe 6 mwezi huu mjini Jericho, huko Ukingo wa magharibi wa mto Jordan, ambapo viongozi wa Israel na Palestina walitofautiana kuhusu maswala ya mipaka, hatima ya mji wa Jerusalem na wakimbizi wa kipalestina.