1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Tanzania itakuwa miongini mwa nchi zinazozalisha mafuta?

Christopher Buke1 Julai 2007

Matokeo ya uvunaji mapipa 90 ya mafuta ghafi nchini humo yanatia matumaini.

https://p.dw.com/p/CHBo
Hii kweli ni mustakabali ya Tanzania?
Hii kweli ni mustakabali ya Tanzania?Picha: AP

Baada ya fununu za muda mrefu za kuwepo dalili za mafuta ya petroli nchini Tanzania hatimaye yamevunwa mapiga 90 ya mafuta yasiyosafishwa, yaani mafuta ghafi, kutoka eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara.

Kwa kweli habari hizi zinaleta matumaini makubwa katika nchi ambayo uchumi wake japo umekuwa ukipanda na kushuka lakini bado haujathubutu kufikia ukuaji wa asilimia 10.

Hata ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha wa 2007/8 ya nchi hii takliban asilimia 40 ya bajeti hiyo inategemea wafadhili wa nje. Sio hivyo tu bali hata makadirio yaliyokuwa yametolewa na wizara husika ili kukidhi mahitaji husika ya bajeti ya mwaka mzima Trilioni zaidi ya 12, serikali ililazimika kukata makadrio hayo hadi nusu yake yaani takliban trilioni 6.

Ndio maana washirika wawili yaani Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC na Kampuni ya Artumas Group Inc, ambao ni wakandarasi na wamiliki wa leseni ya kuendeleza Maeneo ya Gesi ya Mnazi Bay walijitokeza kifua mbele na kueleza mipango kem kem ya kuendeleza utafiti kamili utakaopelekea uzalishwaji kamili wa mafuta ya petroli nchini Tanzania.

Mafuta haya yasiyosafishwa yamevunwa kutoka visima MB 2 na MB 3, eneo hilo la Mnazi Bay. Ama kwa upande mwingine visima hivyo vilizalisha gesi kwa kiwango cha futi za ujazo milioni 10 kwa siku.

Wataalamu wa Artumas wanasisitiza kuwa ni katika visima hivi vikapatikana kiasi kidogo cha vimiminika vya haidrokaboni (liquid hydrocarbons), ambavyo kwa lugha rahisi ndio tunaita mafuta ghafi.

Kadhalika, Artumas Group Inc, ilichimba na kufanya utafiti kwenye kisima kingine MS – IX, na kugundua gesi katika eneo la Msimbati.

Matokeo ya utafiti katika kisima hiki, yanaonesha ulizalishaji wa gesi wa kiwango cha futi za ujazo milioni 9.3 kwa siku, na pia kiasi kidogo cha vimiminika vya haidrokaboni kiligundulika pia katika kisima hiki.

Habari hizi tayari zimezidisha hamu kwa makampuini mengi ya uchimbaji matufa ulimwenguni. Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli Tanzania Bwana Bashiri Mrindoko alisema jumla ya makampuni 10 ya uchimbajij yanaendelea na kazi kwa mujibu wa progamu katika maeneo waliyotengewa ” na kwa ujumla sasa tumetoa leseni 19 za utafiti”.

” Tunaendelea kupata maombi ya kupatiwa maelezo kutoka makampuni ya kimataifa na kwa sasa tunajadiliana na kampuni 3 kwa ajiri ya mikataba ya uchimbaji”, anasisitiza Bwana Mrindoko.

Akizungumzia tathmini yake kuhusu mapiga haya ambayo yamevunwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petrili Tanzania Bwana Yona Kilagane alisema; “ kwa kweli mafuta ni mazuri, yana API kati ya 25 mpaka 27”.

Kiwango hiki cha vimiminika hivyo vilivyozalishwa ni kwa mujibu wa Taasisi ya Petroli ya Marekani (API), ambapo kwa kawaida huhusiana na uwepo wa mafuta ghafi.

Kiasi cha uzalishaji wa vimiminika hivyo vya haidrokaboni, wakati wa majaribio hayo katika visima MB-2, MB-3 na MS-1X kilikuwa jumla ya mapipa 89, katika siku 50 za utafiti wenyewe.

Wataalamu wanazidi kubainisha juu ya Vimiminika hivyo ambavyo sisi twaita mafuta yasiyosafishwa kuwa ni angavu, kana kwamba yametokana na gesi, lakini uzito wake hautofautiani sana na mafuta ghafi, ambayo kwa ujumla huwa na mlolongo mkubwa wa viambata vya haidrokaboni, kuliko kimiminika kilichotokana na mfumo wa gesi.

Katika maeneo mengine duniani, upo ushahidi kwamba vimiminika vya mafuta ghafi haviwi na rangi nyeusi, na hiyo ni kutokana na kutokuwapo kemikali iitwayo asphaltenes, mlolongo mrefu wa haidrokaboni au uchafu katika mafuta. Hii, inaweza pia kuwa ufafanuzi wa rangi angavu ya vimiminika vilivyozalishwa kwenye utafiti huo, katika visima vya Mnazi Bay.

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa kampuni hiyo ya Artumas, Bwana Salvator Ntomola, anasema kutokana na hali hiyo hivi sasa shirika lake linafanya utafiti wa kimaabara, ili kupata jibu zuri zaidi, kuelewa aina ya kimiminika cha haidrokaboni kilichozalishwa kwenye visima vya Mnazi Bay.

Kuonekana kwa vimiminika vya haidrokaboni kwenye visima tajwa wakati wa utafiti huo, kunaonyesha kwamba eneo la Mnazi Bay, na maeneo mengine ya karibu, kama vile Bonde la Ruvuma, yanaweza kuwa na haidrokaboni hizo za vimiminika.

Kwa hiyo wataalamu hao kwa sasa pia wanahaha kuona ikiwa, vimiminika vya haidrokaboni vinatoka kwenye chanzo tofauti na gesi huko ardhini na ama vimiminika vya haidrokaboni vipo katika kiwango kikubwa cha kuweza kuwa cha kibiashara, lakini kama walivyosisitiza wataalam hao mbele za waandishi wa habari “ matokeo yake hadi sasa yanatia moyo”.

Tayari habari hizi zimekaribishwa na wananchi wengi wa Tanzania huku baadhi ya wahariri wa magazeti yachapishwayo nchini wakitahadharisha iangaliwe kwa makini mikataba ambayo serikali inaingia aua itaingia na makampini ya utafiti na uchimbaji madini.