1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je ahadi kubwa za misaada ya maendeleo ni maneno matupu

Josephat Charo5 Februari 2007

Ahadi kubwa kubwa ambazo hazitimizwi. Kila mara linapokuja swala la misaada ya maendeleo mataifa yaliyoendelea kiviwanda ya G8, hutoa ahadi zao. Nchini Ujerumani kansela Angela Merkel anapania kubadili hali hiyo. Ameyapa kipaumbele maswala mapya. Je hiyo ni sababu kuwepo siasa ya maendeleo?

https://p.dw.com/p/CHKl
Alama ya misaada na watoa misaada ya kimaendeleo
Alama ya misaada na watoa misaada ya kimaendeleoPicha: BilderBox

Inakadiriwa kila mtu mmoja katika kila watu sita anaishi katika hali ngumu ya umaskini. Umaskini uliokithiri kwa mujibu wa maelezo ya Umoja wa Mataifa ni kulazimika kuishi kwa kutumia chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku. Kila mara pengo linazidi kupanuka baina ya nchi za eneo la kusini lililo maskini na nchi za eneo tajiri la kaskazini.

Ndio maana Umoja wa Mataifa ulizindua malengo ya milenia ikiwa ni pamoja na elimu ya shule ya msingi, kupunguza idadi ya vifo vya watoto wakati wa uzazi, kuboresha afya ya akina mama, kupambana na ukimwi, malaria na maradhi mengine. Pia malengo hayo yanalenga kuboresha njia za kuyalinda mazingira na kujenga ushirikiano wa maendeleo wa kimatiafa.

Malengo haya ni makubwa na yanagharimu fedha ambazo zinatakiwa kutolewa na mataifa yaliyoendelea kiviwanda. Mataifa hayo yanataka kutoa asilimia 0.7 ya mapato yao ya kitaifa kufikia mwaka wa 2015. Kwa Ujerumani hiyo itakuwa na maana ya kuongeza marudufu kiwango inachotoa kwa wakati huu. Markus Löwe wa taasisi ya misaada ya maendeleo ya Ujerumani hapa mjini Bonn ana wasiwasi ikiwa Ujerumani itaweza kweli kutimiza ahadi yake. Lakini Jeffrey D Sachs, mshauri maalumu wa malengo ya maendeleo ya milenia, anaamini Ujerumani itatimiza ahadi yake.

´Kwa kuchukulia kuwa Ujerumani itayatimiza majukumu hayo pamoja na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya, nafikiri kumekuwa na kutambuliwa kwa makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana mjini Gleaneagles. Kuongezeka kwa misaada hii kulilenga uwekezaji maalumu na wenye manufaa katika nchi maskini, ni sehemu ya haja ya kupunguza umaskini magonjwa na njaa. ´

Stephen Lewis aliyekuwa akifanya kazi na Umoja wa Mataifa kwa miaka 20, na ambaye mara ya mwisho alikuwa mshauri wa maswala ya ukimwi kwa bara la Afrika, anasema Jeffrey Sachs anakubali kiurahisi yaliyosemwa na serikali ya Ujerumani katika mkutano wa Gleneagles nchini Scotland. Anaweza kuwa mkweli lakini tutaona kama hayo yatatimia ifikapo mwaka wa 2015, ameongeza kusema Stephen Lewis. Hata hivyo Lewis anaona kuna mabadiliko makubwa katika sera ya maendeleo ya Ujerumani.

´Msimamo wa kansela wa sasa wa Ujerumani unaonekana wenye nguvu zaidi katika kutoa misaada ili kukidhi mahitaji ya Afrika na mahitaji ya maendeleo ya kimataifa. Hayo ni mabadiliko muhimu ya kimawazo na kimatamshi.´

Kama maneno ya Lewis yatazingatiwa mataifa ya kiviwanda yanatakiwa kulipa asilimia 0.7 ya mapato yao ya kitaifa. Kwa mara ya kwanza kiwango hiki kimefikiwa katika Umoja wa Mataifa katika kipindi cha zaidi ya miaka 35. Tangu wakati huo idadi imekuwa ikiongezeka kupitia maazimio na mikataba ya kimataifa. Hata hivyo ni mataifa machache yanayozingatia maazimio hayo. Norway na Sweden zilitoa asilimia 0.94 ya mapato yao ya kitaifa katika mwaka wa 2005.

´Sidhani tunatakiwa kusubiri hadi mwaka 2015. Kama Wanorway wanaweza kufanya hivyo, leo basi pia mataifa ya G8 yanaweza kufanya hivyo leo.´

Stephen Lewis amesema Norway na Sweden zimedhihirisha kwamba uchumi hauwezi kuathiriwa kwa kutimiza majukumu kwa sehemu nyengine za ulimwengu. Amezitolea mwito nchi za G8 ziige mfano wa nchi hizo.