1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Afrika itafaidika kweli na mkutano wa G8

6 Juni 2007

Vita dhidi ya umasikini na mabadiliko ya hali ya hewa ni mambo mawili yanayokwenda sambamba na yasiyo weza kuachanishwa, wanaharakati wamesisitiza hoja hizo kuwa ni lazima zipewe kipaumbele katika mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za G8 nchini Ujerumani ili maendeleo ya kweli yapatikane barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHD5
Mkutano wa G8 unafanyika nchini Ujerumani
Mkutano wa G8 unafanyika nchini Ujerumani

Iwapo kitisho cha mabadiliko ya hali ya hewa hakitaondoshwa basi ni wazi juhudi zote za kupambana na umasikini kupitia ahadi mbali mbali zitashindwa kufaulu.

Kundi la G8 linazihusisha nchi zilizostawi kiviwanda zikiwemo Uingereza, Canada, Ufaransa, Italia, Japan Urusi, Marekani na Ujerumani ambayo ndio mwenyeji wa mkutano huo na mwenyekiti wa kundi hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Wakuu wa nchi hizo nane wanatarajiwa kuanza mkutano wao wa kilele leo hii katika mji wa Heiligendamm huku maelfu ya waandamanaji ambao wamezuiwa kisheria kusogea karibu na eneo la mkutano huo wakiendeleza pingamizi zao katika mji wa karibu wa Rostock.

Serikali ya kansela Angela Merkel inatarajia kufaulu katika kuundwa itifaki mpya itakayo chukuwa mahala pa itifaki ya Kyoto kwa mujibu wa mfumo wa mwaka 1992 wa umoja wa mataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo muda wake utamalizika mwaka 2012.

Mfumo huo unazitaka nchi za kiviwanda kupunguza utoaji wa gesi chafu zinazo athiri mazingira kwa kiwango cha silimia 5 kuanzia mwaka 1990 hadi kufikia mwaka 2012.

Hata hivyo mapendekezo hayo yanakabiliwa na upinzani wa Marekani ikiwa ndio nchi inayotoa kwa wingi gesi chafu za kiviwanda duniani., huku rais George Bush akipendekeza kuwa nchi 15 zinazotoa gesi chafu za kiviwanda kwa wingi duniani zijadili swala hilo nje ya umoja wa mataifa.

Wanaharakati wa nishati mbadala nchini Afrika Kusini wanazitaka nchi za kiviwanda kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa haraka kufikia kiwango cha asilimia 3o ifikapo mwak 2020 na kupunguza zaidi hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2050.

Iwapo swala la mabadiliko ya hali hewa halitashughulikiwa basi bara la Afrika ndio litaathirika zaidi.

Inakadiriwa kwamba takriban watu milioni 250 watakabiliwa na ukosefu mkubwa wa maji ifikapo mwaka 2020 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa sekta ya kilimo pia itaathirika zaidi katika kipindi hicho.

Waziri mkuu wa Uingereza anaeondoka Tony Blair na ambae anahudhuria mkutano huu wa kilele kwa mara ya mwisho aliwaeleza washiriki katika mkutano uliofanyika katika chuo kikuu cha Afrika Kusini kwamba maafa ya mabadiliko ya hewa huenda pia yakawa chanzo cha kuzidisha usambaaji wa maradhi.

Waziri mkuu wa Uingereza anaeondoka amesema kuwa atawahimiza viongozi wenzake katika mkutano wa G8 watimize ahadi zilizowekwa katika mkutano wa mwaka 2005 wa Gleneagles nchini Scotland.

Shirika la kimataifa la Oxfam katika ripoti yake ya mwezi uliopita limesema kuwa hakuna mabadiliko yoyote katika utoaji wa misaada kwa bara la Afrika bali misaada hiyo ilizidi kupungua kinyume na ahadi zilizowekwa.

Ujerumani wiki iliyopita ilitangaza kuwa imeongeza misaada ya kimaendeleo barani Afrika kwa kiwango cha dola bilioni nne kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2011 huku rais Bush akiahidi kuongeza maradufu misaada ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi kufikia dola bilioni 30 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mkutano huo wa kilele wa wakuu wa nchi wanachama wa kundi la G8 unatarajiwa pia kujadili maswala mbali mbali ya biashara ulimwenguni yaliyokwama na ruzuku kwa wakulima wa nchi za kiviwanda hatua inayo wadhoofisha wakulima wa nchi masikini.

.