ISLAMABAD : Hali ya hatari kuondolewa baada ya mwezi mmoja
10 Novemba 2007Musharraf ametetea utawala wa hali ya hatari kwa kusema kwamba Waislamu wa itikadi kali na kuingilia kati kwa mahkama katika shughuli za kuendesha nchi kutapelekea kujiuwa kwa Pakistan.
Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Benazir Bhutto ameondoka nyumbani kwake mjini Islamabad leo hii baada ya kuwa kwenye kifungo cha nyumbani kwa siku nzima hapo jana ili kumzuwiya asihutubie maandamano katika mji wa karibu wa Rawalpindi kupinga utawala wa hali ya hatari.
Kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi kwenye nyumba ya Bhutto hapo jana ambayo ilizingirwa kwa senyen’ge na vizuizi vyengine vya kangriti.
Sherry Rehman msemaji wa chama cha Bhutto cha PKK anasema chama kizima kimejitolea muhanga hapo kabla kwa ajili ya kurudisha demokrasia na wako tayari kufanya hivyo hivi sasa.Hawataki kumwaga damu katika mitaa ya Islamabad au Pakistan lakini wamefikishwa mahala ambapo hawana jinsi kwamba watapinga ukandamizaji huo kwa nguvu zao zote.
Amri ya kumzuwiya Bhutto nyumbani kwake iliondolewa hapo jana usiku na tayari ametoka nje ya nyumba yake leo hii kuelekea kwenye mikutano na maafisa wa chama chake,viongozi wa vyama vya kijamii na wanadiplomasia wa kigeni.