1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran iko tayari kuzungumza na Marekani

Saumu Mwasimba10 Februari 2009

-

https://p.dw.com/p/GqyG
''Rais Mahmoud AhmedNejad asema enzi ya utawala wa Mabavu Marekani Imekwisha''Picha: AP

Rais wa Iran Mahmoud AhmedNejad akizungumza katika mkutano wa hadhara kuadhimisha miaka 30 ya mapinduzi ya Kiislamu alisema nchi yake inaridhia mabadiliko ya dhati na kwamba iko tayari kuingia katika majadiliano yatakayozingatia mazingira ya usawa na hali ya kuheshimiana.Rais huyo wa Iran mwenye msimamo mkali aliweka wazi kwamba enzi za mabavu zimekwisha na kufungua njia kwa mwanzo mpya wa enzi za maridhiano hivyo basi kitakachokubalika na serikali yake ni mabadiliko ya kweli na wala sio hila.

Msimamo huo wa Iran umejitokeza baada ya hapo jana rais wa Marekani Barack Obama kurudia tena mwito wake wa kutaka paweko mazungumzo ya moja kwa moja na Iran akisema anategemea kuweka masharti ya kufanyika mazungumzo ya aina hiyo katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo.

Hata hivyo nchini Iran maelfu ya wananchi waliojitokeza kuadhimisha miaka 30 ya mapenduzi waliandamana katika barabara za mji mkuu Tehran wakiipinga Marekani.Waandamanaji wakibeba mabango walisikika wakiimba nyimbo zenye maneno ya kuilaani Marekani pamoja na Israeli na kuisifu nchi yao.

Maandamano hayo yamefanyika pia katika miji mingine ya Iran ambapo kwa mujibu wa wizara ya ulinzi kumegunduliwa pia bomu ambalo halijalipuka katika eneo ambalo halikutajwa.Waziri wa ulinzi Gholam Hossein Mohsein Ejeie alisema kuwa vikosi vya usalama vilikuwa macho na kuizima njama ya maadui katika siku muhimu kwa Iran.

Kila mwaka februari 11 Iran inaadhimisha vuguvugu na ushindi uliotokana na mapinduzi ya mwaka 1979 wakati jeshi lilipotangaza ushindi kufuatia kuangushwa utawala wa Sha uliokuwa unaungwa mkono na Marekani.Mwaka huu maadhimisho hayo yanafanyika leo tarehe kumi kwasababu ni mwaka mfupi katika katika Kalenda ya Iran.

Wakati huohuo rais AhmedNejad ametangaza rasmi taifa hilo kuwa taifa lenye nguvu kutokana na mafanikio makubwa ya kisayansi yaliyopatikana na zaidi kutokana na kufanikiwa kurusha satelaiti yake ya kwanza iliyotengenezwa nchini humo.Itakumbukwa kwamba hatua hiyo kubwa ya maendeleo ya kisayansi mnamo februari pili ilizusha hofu kubwa miongoni mwa nchi za magharibi zilizodai kwamba technologia hiyo huenda inaonyesha uwezekano wa Iran kuwa na silaha za maangamizi.Marekani pamoja na nchi nyingine zenye nguvu duniani zinashuku kwamba mpango wa Iran wa Nuklia unaoleta utata unanuiwa kutengeza silaha za kinuklia madai ambayo yanakanushwa na nchi hiyo.