1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watalii Tanzania kuongezeka

30 Juni 2011

Tanzania inatarajia idadi ya watalii watakaoitembelea nchi hiyo mwaka huu kupanda kwa asilimia 13 hadi 26 ikilinganishwa na mwaka wa 2010.

https://p.dw.com/p/11mH8
Tanzania ina vivutio vingi vya utaliiPicha: J. Sorges

Ongezeko hilo linatarajiwa kutokana na mpango mpya wa matangazo wa Tanzania pamoja na nafuu inayotokea baada ya msukosuko wa kiuchumi ulioikumba dunia.

Waziri wa utalii na mali asili wa Tanzania, Ezekiel Maige, alieleza kwamba hapo awali utalii ulikuwa chanzo kikuu cha fedha za kigeni lakini katika miaka miwili iliyopita, madini ndiyo yamechukua nafasi hiyo.

Mwaka 2010 watalii wapatao 794,000 waliitembelea Tanzania, idadi hiyo ikiwa chini ya lengo la kupata watalii Millioni moja. "Kwa sehemu kubwa, hii imekuwa athari ya msukosuko wa kiuchumi," Maige aliliambia shirika la habari la Reuters. "Lengo la serikali ni kuvutia watalii kati ya 900,000 hadi Millioni moja katika mwaka wa 2011. Tunanamini kwamba sasa tuna nafasi nzuri ya kufikia lengo hilo."

Kilimandscharo mit Elefant
Watalii wengi huupanda Mlima KilimanjaroPicha: Das Fotoarchiv

Mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kwa asilimia 11 mwaka 2010 hadi kufikia dola za Kimarekani Billioni 1,28. Ongezeko hilo limepatikana baada ya uchumi wa dunia kustawi.

Licha ya kuwa na vivutio kama mbuga ya wanyama ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote Afrika na kisiwa cha Zanzibar, Tanzania ilishindwa kufikia malengo yake kutokana na miundombinu dhaifu na kwa sababu ya kutokufanya matangazo ya kutosha.

"Tumeongeza  maradufu bajeti ya kuitangaza Tanzania kama eneo la utalii na sasa tunahudhuria zaidi ya maonyesho 25 ya utalii ya kimataifa kwa mwaka ili kuonyesha vivutio vya kipekee vya utalii tulivyonavyo," alisema Maige.

Maige pia alieleza kwamba Tanzania imedhamiria kutumia mvuto wa soka la Uingereza ili kuitangaza zaidi sekta ya utalii. "Vivutio vya utalii vya Tanzania sasa vinatangazwa katika viwanja mbali mbali vya soka Uingereza, miongoni mwao ukiwa uwanja wa Anfield wa timu ya Arsenal pamoja na uwanja wa Manchester City," alisema Waziri huyo.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/ RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman