1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Huwezi kutenganisha maendeleo ya Elimu na maendeleo ya walimu

Haya yamebainishwa na mkutano wa Ubora wa Elimu wa Bagamoyo

Katika mkutano wenye lengo la kuainisha Elimu Bora Tanzania, unaoendelea katika mji wa kitalii wa Bagamoyo, wadau wote kwa pamoja angalau wamekubaliana katika jambo moja kuwa hakuna jinsi ambavyo taifa linaweza kuboresha elimu bila kuboresha maisha ya walimu na kutatua kero zao.

Tofuati ya mawazo inakuja kupatikana pale mtu anapohoji jinsi gani au kwa kiwango gani yaboreshwe maisha ya walimu.

Mkutano huu ambao unawashirikisha wadau wengi wa elimu kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, na kufadhiliwa na Shirika la Oxfam ulilazimika kutembelea baadhi ya shule ili kupata maoni ya walimu, wanafunzi na wazazi.

Jambo lingine ambalo limejitokeza ni kuwa ili kumwezesha mwalimu afundishe kwa moyo ni lazima apate ushirikiano na wazazi na kuwepo mawasiliano ya mara kwa mara baina ya wazazi na walimu, na uongozi wa kamati ya shule.

Hata katika mada iliyowasilishwa na Bi Cheka Omary kutoka Wizara ya Elimu wilayani Bagamoyo alisema kuwa utafiti uliofanywa na watalaamu kutoka ofisi yake unabainisha ukweli huu.

Anaema katika shule ya Kizuiani ambayo jamii ilionekana kuwa karibu na walimu kwa maana ya kuwepo vikao vya kamati ya shule ambayo huwajumuisha walimu wanafunzi na wazazi, ilionekana kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka jana.

Lakini alisema hali ya mambo ilikuwa tofauti kabisa katika shule ya msingi Mlingotini ambapo kumekuwepo na imani za kishirikina kwa miaka mingi huku walimu wanaofundisha katika shule hiyo wakilalamika kuwa wanakabiliana na mambo ya kimiujiza-ujiza.

Anasema walimu hao hulalamika kuwa wakati mwingine mwalimu anapokwenda kulala kitandani usiku anaweza asikie sauti inamwambia ”sogea mbona unanilalia” au kusikia kelele za ajabu ajabu nje ya nyumba na wakati mwingine mtu kutoka usingizini na kukuta amefanya tendo la mapenzi na mtu asiyemfahamu.

Anasema kutokana na hali hiyo walimu wamekuwa wakikaa kwa wasiwasi na matokeo yake shule ya hiyo imefanya vibaya sana katika mtihani wa kumaliza darassa la saba.

Lakini mkutano huu unafanyika katika wakati ambapo serikali ya rais Jakaya Kikwete imekuwa ikikosolewa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya elimu dhidi ya uamuzi uliochukuliwa na serikali hiyo wa kuwachukua watoto waliomaliza kidato cha sita kupatiwa mafunzo ya mwezi mmoja ili wawe walimu katika shule za sekondari.

Uamuzi huo wa serikali ulitokana na idadi kubwa ya watoto kushinda mtihani wa kumaliza darasa la saba lakini kukosa nafasi katika shule za sekondari za serikali.

Baada ya serikali kuamrisha uongozi wa Halmashauri za miji na manispaa kuhakikisha wanajenga shule kwa kushirikiana na wananchi mwaka jana pekee zikapatikana taklibani sekondari 488 lakini tatizo kubwa likawa ni walimu wa kufundisha katika shule hizo.

Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi wa Tanzania Bi Magreth Sitta alifungua mkutano huo hapo jana. Akijua uwepo wa malalamiko ya aina hiyo aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa serikali ya awamu ya nne iliingia madarakani na kukuta hali mbaya sana ya wanafunzi na hivyo haikuwa na cha kufanya ispokuwa kufanya kila linalowezekana.

Alitoa mfano wa shule za Dar es salaam kuwa mwaka 2005 wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba walikuwa ni 35,000 waliofaulu ni vijana 21,000 lakini kati ya hao ni watoto 4,770 waliopokelewa katika shule 12 zilizokuwepo wakati huo.

Waziri aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo kuwa serikali kwa upande mwingine ililazimika kulikazania suala hili kwa kuzingatia kasi inayopigwa na nchi jirani za Kenya na Uganda.

Anasema mwaka 2003 Kenya ilikuwa na jumla ya wanafunzi 862,000 katika sekondari wakati Tanzania ikiwa na wanafunzo 324,000 tu wa sekondari. Anasema uganda mwaka 2005 ilikuwa na taklibani wanafunzi wa sekondari lakini saba wakati tanzania ikiwa na laki tano tu.

Anaongeza kuwa hali hii inatisha kwani Tanzania ina idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na nchi za Kenya na Uganda ambazo zina idadi kubwa ya watoto walio katika shule za sekondari.

Lakini waziri anatetea uamuzi wa serikali kuwa licha ya kuwapa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu hao vijana haitoshi lakini serikali imeweka mikakati ya kuwaendeleza kwa kujiendeleza katika chuo kikuu huria na hata wanapokuwa likizo.

Ama kwa upande wa uboreshaji maisha ya walimu waziri alisema hivi sasa serikali ya awamu ya nne inaangalia namna ya kuboresha mishahara ya wafanyakazi hasa baada ya kuundwa tume ya Kuboresha mishahara ya wafanyakazi ambayo matokeo yake yatawanufaisha hata walimu.

Lakini mbali na tume hiyo anasema tayari wizara yake imempata mtaalamu ambaye ameanza kazi ya kuangalia juu ya ajira ya mwalimu mapato yao na namna ya kuboresha elimu kwa ujumla.

“ tangu mtu anapomaliza chuoni, anapoajiriwa mishahara yake uhamisho wake, upandaji wa madaraja, na yale yote yanayomhusu mfanyakazi, ili tuone jinsi gani ya kupunguza urasimu hasa, ndani ya kazi ya ualimu ambayo imesababisha mambo mengi sana kwa nfamo la kusikitisha zaidi kwa mfano kutokupanda madaraja walimu”.

Baadhi ya mshirika yanayohudhuria semina hii ni shirika la Haki Elimu. Shirika hili limekuwa mkosoaji mkubwa wa sekta ya elimu nchini kiasi mwaka jana serikali ilichukizwa nalo na kulizuia matangazo ya shirika hilo yaliyokuwa yakitolewa katika vyombo vya habari nchini.

Matangazo hayo ya Haki Elimu yalikuwa yakionyesha kasoro mbalimbali zilizo katika mfumo wa elimu.

Bwana Robert Mihayo ni kutoka shirika hilo la Haki Elimu. Aliniambia kuwa hakubaliani na madai yanayotolewa na serikali kuwa wanafunzi walikuwa wengi katika kipindi kifupi na hivyo kuilazimisha kuchukua wanafunzi wa kidato cha sita ili wawe walimu wa sekondari.

“ hili tatizo unajua ni matatizo ya mipango yetu, hawa watoto sio kwamba walizaliwa mwaka jana tu tukajikuta tuna watoto elfu kumi, hapana hawa watoto wamekuwa katika mfumo wamezaliwa tunajua kwamba kuna idadi fulani ya watoto wamezaliwa, na watastahili kupata elimu ya namna fulani, kwa hiyo haya maandalizi yalitakiwa kuwa yamefanyika”, anasisitiza Bwana Mihayo na kuongeza.

“ kwa kweli mimi nina wasiwasi sana, sasa hivi inaonekana tunaelekea zaidi kupata idadi kubwa ya wanafunzi bila kujali kiwango cha ubora wao”.

Mwisho.

 • Tarehe 16.03.2007
 • Mwandishi Christopher Buke
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHlR
 • Tarehe 16.03.2007
 • Mwandishi Christopher Buke
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHlR