1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Watanzania wananyanyaswa kingono nchi za Ghuba

14 Novemba 2017

Shirika la kimataifa la aki za binaadamu la Human Rights Watch limesema wafanyakazi wa ndani wa kike kutoka Tanzania wananyanyaswa kimwili na kingono na wanatumiwa vibaya na waajiri wao katika mataifa ya Ghuba.

https://p.dw.com/p/2naV9
Human Rights Watch Logo

Ripoti hiyo iliyotolewa leo yenye kurasa 100 iliyopewa jina ''Kufanya Kazi Kama Roboti', inaelezea jinsi wafanyakazi wa ndani wa kike kutoka Tanzania wanavyotumiwa nchini Oman na katika Umoja wa Falme za Kiarabu na kwamba wanafanya kazi kwa masaa mengi, hawalipwi mishahara na wanapigwa na wananyanyaswa kingono.

Mtafiti wa shirika hilo lenye makao yake mjini New York, Marekani, Rothna Begum, amesema kuwa wafanyakazi wengi waliowakimbia wafanyakazi au mawakala waliokuwa wakiwanyanyasa wameliambia shirika hilo kuwa polisi au maafisa wa ubalozi wao wamewalazimisha kurudi kwa waajiri wao, la sivyo waache mishahara yao na kutumia miezi mingi kutafuta fedha kwa ajili ya kununua tiketi za kurudi nyumbani.

Nchi za Asia zaimarisha ulinzi

Wafanyakazi wengi wa ndani wanaofanya kazi katika eneo la Ghuba, wanatoka kwenye nchi za Asia, ikiwemo Ufilipino, India na Sri Lanka, lakini kutokana na mataifa hayo kuimarisha ulinzi kwa wahamiaji wao, wafanyakazi wa Afrika wamekuwa wakitumika sana kwenye eneo hilo. Shirika la HRW linakadiria kuwa maelfu ya wafanyakazi wa ndani kutoka Tanzania pekee wako kwenye mataifa ya Ghuba.

Watafiti waliwahoji wafanyakazi 50 wa ndani na kugundua kuwa karibu wote pasi zao za kusafiria zilichukuliwa na waajiri wao wakati tu walipowasili na wanalazimishwa kufanya kazi hadi masaa 21 kwa siku, bila ya kupumzika. ''Wafanyakazi wanasema wanalipwa chini ya kiwango cha pesa walichoahidiwa au hawalipwi kabisa, wanalazimishwa kula chakula kilichooza au mabaki ya chakula, wanafokewa na kutukanwa kila siku na wanafanyiwa ukatili wa kimwili na wananyanyaswa kingono,'' imesema HRW.

Waajiri walijaribu kuwabaka

Imeripotiwa kuwa baadhi ya wafanyakazi hao wa ndani wananyanyaswa kingono na kwamba waajiri wao au ndugu za waajiri hao walijaribu kuwabaka.

Arbeitsbedingungen für Frauen Ethiopische Frau im Libanon bei der Arbeit
Mmoja wa wafanyakazi wa ndaniPicha: AP

Mfumo wa udhamini wa visa unaojulikana kama ''kafala'' pia unazuia uhuru wa wafanyakazi wahamiaji, hali inayowafanya kuwa mateka kwa waajiri wao, huku sheria za ajira zilizopo zikiwa hazitumiwi kwa wafanyakazi wa ndani. Kulingana na mfumo huo, wafanyakazi hao hawawezi kubadili kazi zao bila ya kupata ruhusa kutoka kwa waajiri wao na wanaweza kushtakiwa kwa kosa la 'kutoroka' iwapo watakimbia.

Shirika la Human Rights Watch linasema kuwa serikali ya Tanzania pia inapaswa kulaumiwa, kwani wakati nchi hiyo imeongeza ulinzi kwa wafanyakazi wa ndani ambao ni wahamiaji walioko nchi za nje tangu mwaka 2011, mapungufu katika sera za kuajiri na uhamiaji nchini humo huwaweka wafanyakazi katika hatari kubwa tangu mwanzo na sera hizo zina nafasi ndogo sana ya kufanyiwa marekebisho.

Wakati Tanzania inahitaji kuhakikisha wafanyakazi wa ndani wanatumia mashirika maalum ya ajira yaliyoidhinishwa, mawakala wengi hawajasajiliwa. Aidha mikataba ya kazi inayosainiwa Tanzania haiko kisheria kutumika katika mataifa ya Ghuba. Hata hivyo, Tanzania imesema wafanyakazi wote wanapaswa kupeleka maombi yao ya kuhama kupitia wizara ya ajira ya nchi hiyo, lakini wafanyakazi wengi wanahamia nchi nyingine bila ya kufuata utaraibu huo.

Begum anasema Tanzania inahitaji kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kuhama kwa usalama kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na kwamba nchi hiyo pamoja na Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu, zinapaswa kushirikiana kuzuia wafanyakazi wa ndani ambao ni wahamiaji wasitumiwe vibaya, kuchunguza ukatili wanaofanyiwa pamoja na kuwashtaki wahusika.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Josephat Charo