1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hillary Clinton apigia debe demokrasia Afrika

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amewahimiza viongozi wa kiafrika kuimarisha uhusiano na nchi zinazojali misingi ya demokrasia , na kuzipa kisogo zile zinazoweka mbele tu maslahi ya kibiashara.

Hillary Clinton nchini Senegal

Hillary Clinton nchini Senegal

Ushauri huo wa Bi Clinton kwa viongozi wa Kiafrika, ulitafsiriwa kuilenga China bila kuitaja kwa jina, ambayo imekuwa ikikosolewa na nchi za Magharibi kuweka mbele maslahi yake ya kibiashara barani Afrika, huku ikipuuza masuala mengine muhimu kama vile haki za binadamu na utunzaji wa mazingira.

Aliitoa kauli hiyo mbele ya hadhara ya wanasheria na wanadiplomasia katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, ambako alianzia ziara yake barani Afrika. Bi Clinton alisema kuna maeneo mengi barani Afrika ambako demokrasia inakabiliwa na kitisho, na ambako haki za binadamu hukanyagwa.

''Waafrika wengi bado wanaishi chini ya utawala wa madikteta ambao kwao suala lenye kipaumbele ni kung'ang'ania madarakani kuliko kuinua kiwango cha maisha ya watu wao''. Alisema Hillary Clinton.

Mwisho wa siku za unyonyaji

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton akikutana na kundi la wanawake Senegal

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton akikutana na kundi la wanawake Senegal

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema nchi yake inataka uhusiano na Afrika ambao unazinufaisha pande mbili, na si ule wenye nia ya kuchukua raslimali za bara hilo.

''Siku za wageni kuja barani Afrika na kuchukua utajiri wa bara hilo, bila kuacha chochote nyuma, zimekwisha'' Aliongeza.

Bi Clinton alisema Marekani itazingatia utawala wa sheria na demokrasia, kinyume na nchi nyingine ambazo zinayafumbia macho masuala hayo katika kulinda maslahi yake.

Ushindani wa biashara

Mchambuzi Jackie Cilliers kutoka Taasisi ya Utafiti juu ya Masuala ya Amani iliyopo nchini Afrika Kusini, anasema mtazamo huu mpya wa Marekani kuhusu bara la Afrika, una malengo ya ushindani wa kibiashara.

''Hakuna shaka kwamba ushindani kati ya Marekani na China unaweka ushawishi katika siasa za nje za Marekani. Na ushindani wa kibiashara kati ya China na Marekani barani Afrika unashika kasi. Alipokuwa ziarani nchini Tanzania, Hillary Clinton alisema Afrika inakabiliwa na aina mpya ya ukoloni, ambao unalenga kunyonya raslimali za bara hilo. Alisema Cilliers na kuongeza kwamba hiyo haina tofauti na yale yaliyoyafanywa nchi za magharibi barani Afrika siku za nyuma.'

Nchi za magharibi huishutumu China kupuuza haki za binadamu barani Afrika

Nchi za magharibi huishutumu China kupuuza haki za binadamu barani Afrika

Kauli ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani inakuja baada ya rais wa China Hu Jintao kutangaza mkopo wa dola bilioni 20 kwa nchi za Afrika, na kusema kuwa China ni rafiki wa Afrika ambaye anajali uhuru wa nchi za bara hilo kujichagulia njia ya kufuata katika mchakato wa kujiendeleza.

Katika ziara hii ya siku 11, Hillary Clinton atazitembelea pia Sudan Kusini, Uganda, Kenya na Malawi. Nchi nyingine atakazozizuru ni Afrika Kusini, na Ghana.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com