1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hatimaye viongozi wa Ulaya wafikia makubaliano ya nidhamu

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu katika mkutano wa kilele viongozi wa nchi na serikali za Umoja wa Ulaya mjini Brussels hatimaye wamefikia makubaliano juu ya mpango wa kuweko nidhamu katika bajeti za nchi hizo.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Aidha juu ya hilo wakuu hao pia wameafikiana kuongeza kiasi cha billioni 500 katika mpango mpya wa kuziokoa nchi zinazokabiliwa na mzozo wa kiuchumi katika Umoja huo.Suala la Ugiriki halikuwemo katika agenda ya mazungumzo hayo.

Viongozi wa nchi na serikali za Umoja wa Ulaya hatimae wameidhinisha kwa kauli moja mpango wa kudumu wa nidhamu ya bajeti.Mpango huo kimsingi umepangiwa kuanza kutekelezwa Juli 1 mwaka huu ikiwa ni mwaka mmoja mapema ya ilivyokuwa imepangwa. Mpango huo unaoitwa ESM sasa utachukua mahala pa ule mpango wa zamani unaojulikana kama EFSF na utajumuisha kiasi ya yuro Billioni 500.

Lakini suala la ikiwa kiasi hicho cha fedha kitabidi kuongezwa ni hatua itakayojadiliwa na kuamuliwa mwezi Machi. Serikali ya Ujerumani ilikuwa imeonyesha mwanzoni kutokuwa tayari kuongeza fedha zaidi katika hizo yuro billioni 500 lakini baadae imeonekana kuwa tayari kubadili msimamo wake huo endapo fedha hizo zitahitajika kuongezwa.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.

Aidha viongozi takriban wote wa serikali za Umoja huo wa Ulaya wameafikiana kikamilifu na wazo la kuweko nidhamu ya bajeti isipokuwa Uingereza ambayo tangu mwanzo ilijitenga na mpango huo na Jamhuri Czech.

Hata hivyo nchi hizo mbili huenda zikabidi kulegeza msimamo.Uamuzi wa Ujerumani ulikuwa muhimu zaidi katika suala zima la madeni ya nchi za Umoja huo ikizitaka serikali zote kuheshimu mpango huo uliopangiwa kudumu ili kuepusha msukosuko wa kiuchumi na madeni katika eneo hilo.

Juu ya hilo imewekwa wazi kwamba kuna uwezekano wa serikali kujikuta inaandamwa na sheria mbele ya mahakama ya sheria ya Umoja wa Ulaya ikiwa zitashindwa kuzingatia mkataba huo.

Hata hivyo Ujerumani inahisi kwamba ingekuwa bora zaidi ikiwa kamisheni ya Umoja huo inahusika katika kutoa malalamiko na kuzishtaki nchi zitakazokwenda kinyume na mkataba huo kinyume na ilivyo sasa kwamba nchi binafsi inauwezo wa kufanya hivyo.

''Kitu muhimu katika suala hili ni kuungwa mkono mpango huo uliofikiwa na kamisheni na kuweka wazi kwamba nchi fulani imekwenda kinyume na mkataba wa nidhamu ya bajeti.Ikiwa suala hili litaachiwa nchi husika miongoni mwa wanachama 25 hakuna nchi itakayokuwa tayari kukata rufaa mbele ya mahakama ya sheria. Je kwa hali kama hiyo tunafikiri tutafika mbali.kuna uwezekano tu wa kuzitumbukiza kwenye matatizo nchi zote 25.'' Amesema Kansela Angela Merkel.

Kansela Merkel na Rais Sarkozy

Kansela Merkel na Rais Sarkozy

Mbali na hilo suala jingine lililoibua mjadala ni ushawishi wa nchi ambazo sio wanachama wa kanda inayotumia sarafu ya euro ambazo pia zimeshiriki katika kufikiwa makubaliano ya mpango wa nidhamu ya bajeti za Umoja wa Ulaya. Ufaransa inataka kuona kwamba nchi hizo hazijumuishwi katika mikutano mingine ya kilele itakayofanywa alau mara mbili kwa mwaka.

"Ulaya imeundwa kwa misingi ya makubaliano na kila mmoja ni lazima azingatie makubaliano hayo. Lakini kuna baadhi ya wakati ambapo ikiwa makubaliano hayo yatakwenda mbali basi bila shaka yataporomosha kila kitu na hili ni jambo ambalo sote tunabidi kulifahamu. Na katika Umoja huu kuna mikutano ya daraja tatu kuna mikutano inayozihusisha nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya ambayo inahusu sula zima la soko la ndani. Na pana suala la nidhamu ya bajeti, hapa ni nchi 25 au 26 zinazohusika na panapohusika suala la sarafu ya euro ni wanachama wa kanda inayotumia sarafu hiyo ambao ni 17 ndio wanaohusika." Amesema Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.

Pamoja na kwamba suala la mgogoro wa madeni la Ugiriki halikuwemo ndani ya agenda ya mkutano huo wa kilele lakini liligusiwa japo sio rasmi huku wanachama wengi wa Umoja huo wakiwa wanasubiri kwa hamu ripoti maalum ya pande tatu juu ya suala hilo yaani Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Umoja huo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mwandishi: Hasselbach Christoph
Tafsiri: Saumu Yusuf
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com