1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Tchad kufuatia mapigano ya mwishoni mwa wiki

Hamidou, Oumilkher5 Februari 2008

Waasi wanasema wako tayari kuweka chini silaha,katika wakati ambapo serikali inasema waasi wameshatimuliwa

https://p.dw.com/p/D2yp
Wageni wahamishwa kutoka TchadPicha: AP


 Waasi wa Tchad wanasema wako tayari kukubali silaha ziwekwe chini,baada ya shinikizo la jumuia ya kimataifa,katika wakati ambapo hatima ya wakaazi wa mji mkuu Ndjamena inazidi kuzusha wasi wasi.


"Kwa kutambua usumbufu na shida zinazowapata watchad na kutokana na kuunga mkono juhudi za upatanishi za nchi ndugu za Libya na Burkina Fasso,wanajeshi wa ukombozi wa taifa wanakubali silaha ziwekwe chini haraka"-amesema hayo msemaji wa waasi Abderaman Koulamallah.


Tangazo hilo limetolewa katika wakati ambapo rais wa Tchad aliyejificha ndani ya kasri yake kufuatia mapambano makali ya mwishoni mwa wiki,anajivunia uungaji mkono wa Umoja wa mataifa,Marekani,na mshirika wake mkubwa-Ufaransa.


Wote hao wamelaani mashambulio ya waasi yaliyoanzia january 28 iliyopita nchini Sudan-nchi inayowapatia hifadhi wapinzani wa rais Deby.Serikali ya mjini Khartoum inatuhumiwa kutaka kufuja juhudi za kupelekwa wanajeshi 3700 wa umoja wa ulaya katika nchi jirani na Sudan ili kuwalinda wakimbizi wa Darfour na watu walioyapa kisogo maskani yao kufuatia mapigano.


Waasi wanakiri kwamba shinikizo la kidiplomasia kutoka nchi za nje kutaka silaha ziwekwe chini, lilikua kubwa mno.


Waasi wamelaani wakati huo huo kuingilia kati jeshi la wanaanga la Ufaransa lililosababisha hasara miongoni mwa raia wa kawaida.


Jeshi la Ufaransa limekanusha lakini madai hayo.


Waziri mkuu wa Tchad Nourredin Delwa Kassiré Coumakoyé,amepinga fikra ya kuweka chini silaha akihoji waasi "wameshindwa".


Hata hivyo sauti zimezidi makali mjini Paris nchini Ufaransa.Rais Nicolas Sarkozy amesema hii leo tunanukuu:"Ikiwa Ufaransa itabidi kutekeleza jukumu lake,basi haitachelea"Mwisho wa kumnukuu.


Juhudi za kidiplomasia zimechochewa pia na hofu kuhusu hali ya raia wa kawaida,waliojeruhiwa au walioyapa kisogo maskani yao.


Watu wasiopungua elfu moja wamejeruhiwa kufuatia mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi .Hayo ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu lililozizunguka hospitali za mji mkuu Ndjamena.


Watchad wanazidi kuuvuka  mto Chari na kukimbilia Cameroun.Wakimbizi hadi 20 elfu wameandikishwa hadi sasa huko Kousseri-mji wa Kameroun ulioko upande wa pili wa mji mkuu wa Tchad-Ndjamena.


Maria-Theresa Garrido wa shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu nchini Cameroun anasema:


"Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu linashirikiana na jumuia ya  msalaba mwekundu nchini Tchad.Wanazunguka kila mahala katika mji mkuu kuwakusanya majeruhi na kuwapeleka hospitali au katika shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu.


Wakati huo huo ofisi za umoja wa mataifa zimeporwa na nyengine kutiwa moto kufuatia mapigano mjini  Ndjamena.






►◄