Haki za watoto zapewa kipaumbele | Masuala ya Jamii | DW | 23.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Haki za watoto zapewa kipaumbele

Nchi 47 wanachama wa baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa wiki hii zimefikia makubaliano juu ya swala la haki za watoto na kuibuka tafauti zilizokuwepo katika mijadala ya hivi karibuni huko mjini Geneva.

Wajumbe katika ukumbi wa baraza kuu la umoja wa mataifa

Wajumbe katika ukumbi wa baraza kuu la umoja wa mataifa

Katika mjadala wa sasa ulioanza machi 12 na unaoaendelea hadi machi 30 wanachama wanafanya mjadala maalumu kuhusu ripoti iliyotolewa na mtalaam wa umoja wa mataifa wa kibinafsi juu ya hatua zitakazochukuliwa kudhibiti mateso dhidi ya watoto.

Ripoti ya mtalaam huyo kutoka Brazil Paulo Pinheiro kwa mara ya kwanza iliwasilishwa katika baraza kuu la umoja wa mataifa mwezi October mwaka 2006 na mtaalamu huyo anatarajiwa kuwasilisha mafuatilizo ya ripoti hiyo mwezi Septemba.

Jambo muafaka ni kuwa nchi wanachama zimeweka kando tafauti zao na kuunga mkono ripoti hiyo inayozingatia haki za watoto.

Katika ripoti hiyo mtalaamu huyo Pinheiro ametilia mkazo mapendekezo yatakayoziwezesha sheria za kukinga na kuwajibika pindi haki za watoto zitakapokiukwa.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kudumishwa haki za watoto kuanzia nyumbani, katika jamii, mashuleni, kwenye jela za watoto na makao ya watoto na pia katika maeneo ya kazi.

Lakini hata hivyo mapendekezo ya mtalaam Paulo Sergio Pinheiro hayajumuishi haki za watoto katika maeneo ya mizozo ijapokuwa amegusia mweleko sawa na kutoa mfano wa mzozo wa Palestina.

Amesema katika ripoti yake kuwa dhulma dhidi ya watoto zinaweza kukingwa katika nchi na serikali mbali mbali zitakaposisitiza juu ya haki za watoto na kuhakikisha kuwa watoto wanapata mahitaji yao muhimu akitilia maanani msaada kwa familia ili kufanikisha malezi bora ya watoto.

Ripoti hiyo imeshauri juu ya kuteuliwa mjumbe maalum atakaesimaia swala la mateso dhidi ya watoto.

Mjumbe huyo atahitajika kushughulikia mapendekezo hayo ikiwa ni pamoja kutia mkazo katika mfumo wa sheria, utendaji wa ndani katika kila nchi na kutafuta mfumo utakao wawezesha watoto kushiriki ili kuwezesha mawazo yao kusikilizwa.

Cecile Trochu msimamizi wa mpango wa shirka la kupambana na mateso dhidi ya watoto duniani OMTC amesema wazo la kuteuliwa mjumbe maalum atakaeshughulikia mateso dhidi ya watoto linaungwa mkono na wengi.

Mfumo wa sasa wa umoja wa mataifa juu ya kupambana na mateso dhidi ya watoto hauambatanishi kifungu cha mateso dhidi ya watoto majumbani au katika taasisi na hasa katika asasi za kisheria.

Mjumbe kutoka Uruguay amependekeza pia liangaliwe swala la watoto na jinsi wanavyohusishwa katika ukahaba na kushirikishwa katika picha za ngono pamoja na biashara ya kuwauza watoto.

Ujumbe wa Uruguay unapanga kujadili ripoti hiyo ya mtalaam Pinheiro ambayo ilimulikwa na rais wa baraza Luis Alfonso de Alba.

Kwa kipindi cha miaka kumi Uruguay imekuwa ikidhamini maazimio juu ya haki za watoto katika makao makuu ya umoja wa mataifa mjini Geneva na katika baraza kuu la umoja wa mataifa huko New York.

Lakini katika majadiliano haya ya sasa Uruguay inaiwakilisha Latin Amerika na Caribbean.

Kwa mujibu wa mtaalmu Pinheiro anasema katika Latin ya Amerika shida inayojitokeza ni kwamba kubadilika kwa mfumo watawala za kidikteta za kijeshi hadi kuelekea demokrasia katika nchi nyingi mnamo miaka ya themanini na tisini, hatua hiyo haikuleta mabadiliko makubwa katika demokrasia na haki za watoto na vijana.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com