1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Guterres asikitishwa na kuanza upya kwa vita Ukanda wa Gaza

1 Desemba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonyesha kusikitishwa na kuanza upya kwa vita katika Ukanda wa Gaza baada ya makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas kukamilika mapema Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4ZgCw
Israel yaanza mashambulizi Gaza dhidi ya Hamas baada ya makubaliano ya muda mfupi ya usitishaji vita kumalizika. Disemba 1, 2023.
Israel yaanza mashambulizi Gaza dhidi ya Hamas baada ya makubaliano ya muda mfupi ya usitishaji vita kumalizika. Disemba 1, 2023.Picha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema watu wasiopungua 32 wameuawa katika saa tatu za kuanza kwa mapigano Ijumaa. 

Kupitia mtandao wa kijamii, Guterres ameandika kuwa "ninasikitika sana kwamba operesheni za kijeshi zimeanza tena huko Gaza. Bado ninatumai kuwa itawezekana kurefusha muda wa makubaliano yaliyokuwepo.” Guterres ameongeza kuwa kuanza tena mashambulizi kunaonyesha tu jinsi ilivyo muhimu kuwa na usitishaji kamili wa vita kwa misingi ya kibinadamu."

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Volker Türk amefananisha hatua ya kuanza kwa vita huko Gaza na "janga".

 

Kwenye taarifa aliyotoa leo Ijumaa mjini Geneva, Türk amesema hali katika Ukanda wa Gaza "ni zaidi ya mgogoro" kwani Wapalestina zaidi wako katika hatari ya kuuawa au "kulazimika kuhamia sehemu za Gaza ambazo tayari kuna msongamano mkubwa wa watu na pia sio safi.

Matamshi ya waziri mkuu wa Uhispania kuhusu Gaza yaikasirisha Israel

Kupitia msemaji wa shirika hilo la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani, Türk ametaka juhudi kuongezwa kurejesha makubaliano ya usitishaji vita. "Kuanza tena kwa vita huko Gaza ni janga. Ninaomba pande zote na Mataifa yenye ushawishi juu ya pande husika kuongeza juhudi, mara moja, ili kuhakikisha usitishaji mapigano - kwa misingi ya kibinadamu na haki za binadamu."

Antonio Guterres| Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Guterres: Kuanza tena mashambulizi kunaonyesha tu umuhimu wa kuwa na usitishaji kamili wa vita kwa misingi ya kibinadamu.Picha: Brendan McDermid/REUTERS

Marekani yataka Israel kuwawajibisha watakaochochea mashambulizi dhidi ya raia

Hayo yakijiri, Marekani inaandaa orodha ya walowezi wa Kiyahudi watakaopigwa marufuku kusafiri na kuingia nchini humo kwa kuhusika na mashambulizi Ukingo wa Magharibi.

Hayo yamesemwa na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani.

Jana Alhamisi waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alimwambia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na maafisa wake kwamba utawala wa Marekani unategema serikali ya Israel kuwawajibisha walowezi watakaotuhumiwa kufanya mashambulizi kama hayo, lakini Marekani pia haitasita kuchukua hatua kama hiyo kivyake. Ni kulingana na maelezo ya afisa wa ngazi ya juu wa Israel ambaye alizungumza kwa sharti la kutotambulishwa.

Netanyahu na vita mbili zinazomkabili - Hamas na nyumbani

Israel ilirejea vitani mjini Gaza mapema Ijumaa baada ya makubaliano ya muda mfupi ya usitishaji vita baina yake na kundi la Hamas kukamilika. Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema watu wasiopungua 32 wameuawa katika saa tatu za kuanza kwa mapigano Ijumaa.

Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas baada ya kundi hilo kuishambulia mnamo Oktoba 7, 2023.
Wanajeshi wa Israel wakiwa juu ya kifaru cha kivita mnamo Novemba 23, 2023 wakati wa vita vyake dhidi ya kundi la Hamas.Picha: Amir Cohen/REUTERS

Israel na Hamas zaelekezeana lawama kwa kuvunjika kwa makubaliano

Israel ilililaumu kundi la Hamas kwa kukiuka makubaliano hayo ikidai mifumo yake ya ulinzi wa angani, ilizuia roketi iliyodaiwa kurushwa kutoka Ukanda wa Gaza, ambao ni makao ya Hamas, kundi ambalo Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeliorodhesha kuwa la kigaidi.

Hamas kwa upande wake pia inailaumu Israel kwa kuvunjika kwa makubaliano hayo likisema ilikataa masharti ya kuwaachilia mateka zaidi.

Qatar ambayo ndiyo mpatanishi mkuu, imesikitikia kuanza tena kwa mashambulizi ya Israel, lakini imesema juhudi za kurejesha makubaliano ya usitishaji vita zinaendelea.

Wanajeshi wa Israel wakitizama picha za watu waliouawa na walioshikwa mateka baada ya shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023.
Wanajeshi wa Israel wakitizama picha za watu waliouawa na walioshikwa mateka baada ya shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023. Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Israel yasema watu 125 wangali wanashikwa mateka Gaza

Katika muda wa siku saba ambapo makubaliano hayo yalidumu, zaidi ya mateka 100 waliachiliwa huru. Israel imesema takriban watu 125 wangali wanashikiliwa mateka.

Aidha Israel iliwaachilia wafungwa wa Kipalestina 240 waliokuwa kwenye magereza yake kama sehemu ya makubaliano hayo.

Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas, baada ya wanamgambo hao wa Kiislamu kufanya shambulizi baya la kushtukiza mnamo Oktoba 7, kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200 na kuwashikilia mateka zaidi ya watu 240.

Tangu vita vilipoanza Ukanda wa gaza, wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema idadi ya watu waliouawa imefika 15,000.

Vyanzo: DPAE, APAE