1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

UN: Haiti yahitaji msaada wa kimataifa kudhibiti uhalifu

Lilian Mtono
16 Agosti 2023

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameiomba jamii ya kimataifa kupeleka kikosi maalumu cha kimataifa kitakachojumuisha wanajeshi na polisi nchini Haiti kukabiliana na magenge ya uhalifu.

https://p.dw.com/p/4VDXe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema matumizi ya nguvu yanaweza kuisaidia Haiti kukabiliana na uhalifu.
Umoja wa Mataifa unahimiza jamii ya kimataifa kuisaidia Haiti ili kurejesha hali ya usalama.Picha: Eskinder Debebe/UN/XinHua/dpa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito huu wakati raia nchini humo wakiyakimbia makazi yao kutokana na kuongezeka kwa visa vya uhalifu na hasa katika mji mkuu Port-au-Prince. 

Kwenye barua yake ya kurasa 12 kwa Baraza la Usalama la umoja huo, iliyoonwa na shirika la habari la AP, Guterres amesema kwamba kushughulikia hali ya usalama nchini Haiti kunahitaji hatua kali na pana zitakazorejesha utekelezwaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu katika operesheni za polisi dhidi ya magenge yenye silaha kali.

Barua hiyo ilikuwa inajibu kwa azimio la Baraza la Usalama lililopitishwa Julai 14, lililompa siku 30 Guterres kuja na chaguo kamili litakalosaidia katika kupambana na magenge yenye silaha nchini Haiti.

Guterres ililikaribisha ombi la Kenya la kuongoza kikosi cha kimataifa pamoja na kuzungumzia kwa mara nyingine ahadi ya msaada zaidi kutoka Bahamas na Jamaica, pamoja na Antigua na Barbuda huku akizitaka nchi nyingi zaidi na hasa Marekani kuchangia katika mkakati huu wa sasa.

Magenge ya uhalifu yamelielemea jeshi la polisi nchini Haiti, huku wachambuzi wakikadiria kwamba kwa sasa magenge hayo yanadhibiti karibu asilimia 80 ya Port-au-Prince. Kulingana na Guterres, magenge hayo yameuzunguka mji huo na kuziba barabara zinazotokea kaskazini mwa taifa hilo, kusini na mashariki na machafuko yanasambaa hadi kwenye mkoa wa Artibonite, katikati mwa Haiti, hatua inayozuia ufikishwaji wa misaada na bidhaa.

Soma Zaidi: Guterres: jeshi la kimataifa linapaswa kupelekwa Haiti

Pichani ni kiongozi wa kundi la kijamii la Bwa Kale Nertil Gewalt akigawa mapanga kwa raia kama mkakati wa kukabiliana na makundi hayo ya kihalifu.
Haiti inakabiliwa na uhalifu unaofanywa na magenge hasimu hali inayowafanya raia kuishi kwa mashaka makubwa.Picha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Wakaazi wayakimbia makaazi yao kunusuru maisha yao.

Jana Jumanne, baadhi ya familia zililazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano baina ya magenge hayo, zikichukua vitu vichache tu wakati ripoti zikisema karibu watu 190,000 wamelazimika kukimbia tangu mwaka uliopita. Miongoni mwa waliokimbia ni Dorleans Michjoe: ambaye hata hivyo, hakuyalaumu magenge hayo, na badala yake aliigeukia serikali akisema "Halikuwa genge la Tilapli or Bougoy walionifukuza nyumbani kwamba, ilikuwa ni serikali iliyonifukuza na serikali ya Haiti ambayo inawaua raia wake wote unaowaona.. kwa sababu ni serikali ambayo ina kile inachoita uhalali wa vurugu. Serikali inaweza kuona genge la Grand Ravine likichukua udhibiti wa mtaa na isifanye chochote."

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch limetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuingilia haraka ili kumaliza kadhia hiyo. Haiti inayokaliwa na watu zaidi ya milioni 11 ina polisi karibu 10,000 tu na zaidi ya watu 30 walikuwa wameuawa tangu mwezi Januari hadi Juni, hii ikiwa ni kulingana na shirika hilo.

Kulingana na Guterres, magenge hayo yamekuwa yakiwapiga watu risasi kwenye maeneo ya umma na majumbani kwao, kuwachoma moto watu walioko kwenye vyombo vya usafiri, kuwakatakata viungo na kuwanyoa wapinzani wao, kuwafunza watoto kupigana na kuwanyanyasa kijinsia na kuwabaka wasichana na wanawake. 

Waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry alituma mwito wa dharura Oktoba mwaka uliopita akiomba kupelekwa haraka kwa vikosi maalumu vilivyojihami kwa silaha ili kuyakabili magenge hayo. Hata hivyo hakukua na taifa lililojitolea kuongoza kikosi kama hicho hadi Kenya ilipoamua kufanya hivyo, mwishoni mwa mwezi Julai.

Soma Zaidi: Haiti yakubali pendekezo la kupokea kikosi cha askari wa Kenya